Wizara ya Afya Gaza: Kukatwa umeme kutasababisha maafa makubwa katika hosiptali
Oct 12, 2023 00:11 UTC
Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imetangaza kuwa kukatwa umeme katika eneo hilo, lililowekewa mzingiro na marufuku ya kila kitu na utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel, kutasababisha vifaa vya mahospitali vishindwe kufanya kazi na kuhatarisha maisha ya wagonjwa wa Kipalestina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la SAMA, Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imesema: kukatwa umeme katika ukanda huo na utawala haramu wa Kizayuni kutasababisha mashine za kuua viini vya maradhi na vituo vya usambazaji oksijeni na maji katika hospitali vishindwe kufanya kazi.
Wizara hiyo imebainisha kuwa: kukatwa umeme kutapelekea kusimamishwa pia huduma za kusafisha damu na kupoteza maisha wagonjwa wa figo 1,100, ikiwa ni pamoja na watoto 38 wanaohitaji usafishaji mara tatu kwa wiki. Maisha ya watoto 100 wanaozaliwa kabla ya wakati katika wodi za watoto nayo pia yako hatarini kutokana na kukatika umeme katika vituo vya afya.

Taasisi hiyo ya tiba ya Palestina imeongezea kwa kusema: "kukatwa umeme kutasimamisha huduma za maabara 58 na benki za damu. Wakati huohuo, maelfu ya watu waliojeruhiwa na wagonjwa wanahitajia sana kufanyiwa vipimo vya kitiba na kutiwa damu mwilini, kwa hiyo kukatika umeme kutasimamisha huduma za uchunguzi zinazofanywa na timu ya matabibu kuhusiana na majeraha waliyopata majeruhi hao."
Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imeendelea kueleza katika taarifa kwamba shida ya umeme itasababisha pia lifti zisifanye kazi na kwa sababu hiyo, itakuwa vigumu kuhamisha wagonjwa wa kliniki na majeruhi hospitalini.
Ifahamike kuwa mashambulio ya kinyama ya anga ya utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza yangali yanaendelea huku utawala huo ghasibu ukifanya jinai za mauaji ya kimbari kama ilivyo kawaida yake ya kila mara na kuendelea kutenda jinai dhidi ya Ukanda wa Gaza kwa kutumia mabomu yenye fosforasi mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa. Kutokana na mashambulizi hayo, Wapalestina 1,100 wameshauawa shahidi hadi sasa na wengine 5,184 wamejeruhiwa.../