Saudi Arabia yatangaza sharti la kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel
Saudi Arabia imetangaza sharti la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel wakati huu jeshi la Israel likiendelea kufanya mauaji ya umati dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Hayo yameelezwa na Khalid al-Falih Waziri wa Uwekezaji wa Saudi Arabia katika mkutano katika Jukwaa la Uchumi Mpya la Bloomberg lililofanyika Singapore, na kusisitiza kwamba, kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ni ajenda ambayo bado iko mezani lakini kwa sharti la kufikiwa utatuzi wa amani kwa suala la Palestina.
Waziri wa Uwekezaji wa Saudi Arabia, ameongeza kuwa, suala la Saudia kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel lingali mezani na ni wazi kwamba kipigo cha mwezi uliopita kimeonyesha ni kwa nini Saudi Arabia inasisitiza kwamba utatuzi wa mzozo huo lazima liwe ni sehemu pana zaidi ya uanzishaji uhusiano wa kawaida na Israel katika Mashariki ya Kati.
Waziri huyo wa uwekezaji wa Saudia amebainisha kuwa, "Haki za kimsingi za watu wa Palestina zimenyakuliwa na hawajapewa haki ya kuunda nchi na kuishi kwa amani, na sasa umewadia wakati wa hali hii mbaya (kuzidi kuwa mbaya hali ya Gaza) kuzingatiwa na maudhui hii ya utatuzi wa mgogoro.
Licha ya kuwa hadi sasa hakuna uhusiano rasmi baina ya Israel na Saudi Arabia, lakini pande hizo mbili hususan kuanzia mwaka 2020, zimechukua hatua katika mkondo wa kupanua wigo wa ushirikiano wao.
Serikali ya Riyadh mwaka jana ilifungua anga yake kwa ajili ya ndege za Israel, na hivi karibuni, irihusu ndege ya Air Sychelles iliyokuwa imebeba abiria 128 wa utawala huo pandikizi kuelekea Tel Aviv, kutua mjini Jeddah eti baada ya kupatwa na hitilafu za kiufundi.