Hizbullah ya Lebanon: Tutaendelea kuwaunga mkono watu wa Gaza na Muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i104586-hizbullah_ya_lebanon_tutaendelea_kuwaunga_mkono_watu_wa_gaza_na_muqawama
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imesisitiza kuwa itaendelea kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Gaza na Muqawama wao.
(last modified 2026-05-19T09:45:50+00:00 )
Nov 10, 2023 03:26 UTC
  • Hizbullah ya Lebanon: Tutaendelea kuwaunga mkono watu wa Gaza na Muqawama

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imesisitiza kuwa itaendelea kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Gaza na Muqawama wao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, harakati ya Hizbullah ya Lebanon ilitangaza jana kuwa katika mwendelezo wa uungaji mkono wake kwa wananchi wanamuqawama wa Palestina na Muqawama wake wa kishujaa, wapiganaji wake wa muqawama wa Kiislamu wameshambulia eneo la al-Mutla kwa makombora yanayoongozwa kwa mitambo na kusababisha hasara na maafa kwa Wazayuni.

Kwa upande mwingine, duru za habari zimeripoti kuwa kufuatia shambulio hilo la makombora king'ora cha indhari ya hatari kilisikika katika ngome ya kijeshi ya Shatula huko Al-Jalil Magharibi, kwenye mpaka wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Lebanon.

Wakati huohuo, televisheni ya Al-Mayadeen imetangaza kuwa, jeshi la Kizayuni limeshambulia kwa makombora eneo la Kafarkala, Addisseh na Deir Mimas kusini mwa Lebanon.

Ngome za kijeshi za Zariyat na Miskaf Aam kwenye mpaka wa pamoja wa Lebanon na Palestina inayokaliwa kwa mabavu nzao pia zimeshambuliwa na wanamapambano wa Muqawama.

Vyombo vya habari vya Kizayuni navyo pia vimeripoti kusikika milio ya king'ora cha tahadhari ya hatari katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya Shtola na Ifen Menachem karibu na mpaka wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Lebanon.

Katika ripoti nyingine, Al-Mayadeen imetangaza kuwa vikosi vya wavamizi wa Kizayuni vimeshambulia eneo lililopo kati ya Ramieh na Beit Leif katika sehemu ya magharibi ya kusini mwa Lebanon.

Televisheni hiyo imeripoti kuwa yamezuka mapigano kati ya wanamapambano wa Muqawama na askari wa Kizayuni katika ngome ya kijeshi ya wavamizi hao ya Miskaf Aam kwenye mpaka wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Lebanon.

Al-Mayadeen imeripoti pia kwamba mizinga ya jeshi la utawala wa Kizayuni imelenga kandokando ya kitongoji cha al-Quzah kusini mwa Lebanon.../