Hamas: Gaza haitatawaliwa na yeyote isipokuwa wakazi wake
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i104706-hamas_gaza_haitatawaliwa_na_yeyote_isipokuwa_wakazi_wake
Afisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amepuuzilia mbali madai ya utawala haramu wa Israel na baadhi ya waungaji mkono wake wa Magharibi kuhusu Gaza kutawaliwa na mamlaka iliyo nje ya eneo hilo baada ya kumalizika vita vya maangamizi ya umati vinavyoendelezwa na Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 13, 2023 02:31 UTC
  • Hamas: Gaza haitatawaliwa na yeyote isipokuwa wakazi wake

Afisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amepuuzilia mbali madai ya utawala haramu wa Israel na baadhi ya waungaji mkono wake wa Magharibi kuhusu Gaza kutawaliwa na mamlaka iliyo nje ya eneo hilo baada ya kumalizika vita vya maangamizi ya umati vinavyoendelezwa na Israel.

Osama Hamdan, ambaye ni mwakilishi wa Hamas nchini Lebanon na pia mwanachama wa ofisi ya kisiasa ya harakati hiyo, ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari Jumapili mjini Beirut.

Hamdan ameongeza kuwa: "Tunauambia utawala wa Marekani na viongozi wahalifu wa utawala vamizi wa Israel kwamba Gaza itaongozwa na watu wake tu, na hakutakuwa na mamlaka ya kisiasa au kiusalama isipokuwa ya Wapalestina wa eneo hilo..

Matamshi yake yamekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kusema mapema wiki iliyopita kwamba vita vya Israel dhidi ya Gaza vitakapomalizika, eneo hilo linapaswa kuunganishwa na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu chini ya utawala wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Hata hivyo, siku ya Jumamosi Waziri Mkuu wa utawala dhalimu Israel Benjamin Netanyahu alipinga kurejeshwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina huko Gaza huku akisisitza kuwa lazima Gaza itawaliwe na mfumo tofauti.

Hospitali ya Al Ahri Arab baada ya hujuma ya kinyama ya Israel

Hamdan amewajibu Wamarekani na Wazayuni kwa kusema: "Sisi ni watu huru ambao hatukubali utawala kutoka kwa mtu yeyote, na damu yetu na maisha yetu ndiyo gharama ya uhuru wetu."

Kwingineko katika matamshi yake, afisa huyo wa Hamas ameikosoa jamii ya kimataifa kwa kutofanya lolote kujibu mashambulizi ya anga ya Israel kwenye hospitali ya al-Ahli Arab, inayojulikana pia kama Hospitali ya Baptist, mwezi uliopita.

Afisa huyo wa Hamas amebainisha kuwa: "Wanazi mamboleo walio katika utawala wa Israel… walifanya mauaji katika Hospitali ya Baptist katika Jiji la Gaza mnamo tarehe 17 Oktoba, ambapo takriban watu 500 waliuawa shahidi na takriban raia 600 na watoto walijeruhiwa. Ulimwengu haukuhoji jinai hiyo ya Israel, wala haukuwawajibisha wahalifu wake."

Ameongeza kuwa badala ya kuilaani Israel, baadhi ya wafuasi na waungaji mkono wa utawala huo haramu hata waliihimiza Israel kuendeleza jinai zaidi dhidi ya Wapalestina.