Wabahrain waandamana kumuunga mkono Sheikh Qassim
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i10489-wabahrain_waandamana_kumuunga_mkono_sheikh_qassim
Kwa mara nyingine tena wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano ya kuonyesha uungaji mkono wao kwa mwanachuoni mkubwa wa Kiislamu, Ayatullah Sheikh Isa Qassim ambaye hivi karibuni alivuliwa uraia na utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 03, 2016 03:05 UTC
  • Wabahrain waandamana kumuunga mkono Sheikh Qassim

Kwa mara nyingine tena wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano ya kuonyesha uungaji mkono wao kwa mwanachuoni mkubwa wa Kiislamu, Ayatullah Sheikh Isa Qassim ambaye hivi karibuni alivuliwa uraia na utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain.

Maandamano hayo yalifanyika jana jioni katika kitongoji cha Diraz, kaskazini magharibi mwa nchi ambapo waandamanaji walisikika wakipiga nara za kuulani utawala wa Aal-Khalifa kwa kitendo chake hicho.

Maandamano mengine ya kumtetea Ayatullah Qassim sawa na kushinikiza uhuru wa kijieleza na demokrasia nchi humo yamefanyika usiku kucha katika kisiwa cha Sitra na pia katika kijiji cha Nuwaidrat. Maafisa usalama wa utawala wa kifalme wa Manama wametumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamebeba mabango yenye picha za Sheikh Qassim. Wiki iliyopita, wananchi wa Iraq walifanya maandamano katika mji mkuu Baghdad na mji wa Basra, kuonyesha uungaji mkono wao kwa mwanachuoni huyo.

Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu imelaani hatua ya utawala wa Aal-Khalifa kumvua uraia mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu nchini Bahrain Ayatullah Sheikh Isa Qassim. Kadhalika Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni baadhi ya nchi na asasi za kimataifa zilizotoa taarifa ya kulaani kitendo cha kupokonywa uraia Ayatullah Qassim, kwa madai kuwa ametumia vibaya nafasi yake kwa maslahi ya madola ya kigeni.