Ombi kwa ICC kuchunguza jinai za kivita za Israel huko Gaza
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai za Kivita ya The Hague ICC ametangaza habari ya kupokea maombi ya nchi 5 kwa ajili ya kuchunguzwa jinai za kivita za utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza.
Karim Khan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, amesema: Maombi hayo yamewasilishwa na Afrika Kusini, Bangladesh, Bolivia, Comoro na Djibouti. Taarifa ya ofisi ya mwendesha mashtaka huyo imesema: Ofisi hii imekusanya ushahidi na nyaraka nyingi kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Nchi tano hizo zimeitaka Mahakama ya kimataifa kuchunguza jinai za kivita za utawala wa kigaidi wa Israel huko Gaza. Awali Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alitangaza kuwa ameushtaki utawala wa Kizayuni katika Mahakamu ya Kimataifa ya jinai kwa kutekeleza jinai katika vita vyake vya kikatili huko Gaza. Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naldi Mandisa Pandour pia amesema: Ulimwengu lazima uilazimishe Israel kukomesha jinai zake dhidi ya binadamu huko Gaza. Afisa huyo wa Kiafrika ameongeza kuwa: 'Israel ni mamlaka inayokalia kwa mabavu ardhi za Palestina hivyo lazima iheshimu Mkataba wa Geneva; Israeli haiwezi kutangaza vita dhidi ya watu inaokalia kwa mabavu ardhi zao.'
Jumuiya ya Waarabu ya Haki za Binadamu nchini Uingereza katika ombi lililotiwa saini na makumi ya shakhsia wa kisiasa, kisheria na kitaaluma, imemtaka mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kushughulikia hali mbaya ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na jinai zinazofanywa na utawala haramu wa Kizayuni katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Waliotia saini barua hiyo pia wamemtaka Karim Khan, kushughulikia kesi za jinai za Wazayuni dhidi ya taifa la Palestina zilizowasilishwa kwenye mahakama hiyo miaka 9 iliyopita.
Ijapokuwa vitendo vya kikatili na kinyama vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina daima vimekuwa vikilaaniwa mara zote na mashirika ya kutetea haki za binadamu na taasisi za kimataifa, lakini vita vya sasa huko Gaza na mauaji ya kimbari na kikatili ya wanawake na watoto yamezifanya nchi mbalimbali kwa mara nyingine tena kuitaka mahakama hiyo ya kimataifa kufanya uchunguzi kuhusiana na suala hilo.
Katika Kifungu cha 8 cha Mkataba wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, kesi kama vile mauaji ya makusudi, kuwekwa kizuizini au kuteswa, kusababisha mateso au majeraha makubwa katika mwili au afya, uharibifu mkubwa wa maeneo ambayo hayatumiki kijeshi, kuhamishwa au kufungwa raia kinyume cha sheria, kushambulia au kulipuliwa kwa mabomu miji, vijiji, na maeneo ya makazi ambayo si malengo ya kijeshi pamoja na kusababisha njaa kwa raia, ni mifano ya wazi ya jinai za kivita. Kwa kuzingatia hilo, kile ambacho Israel inakifanya katika maeneo inayoyakalia kwa mabavu, hasa huko Gaza, ni mfano wa wazi wa jinai zilizotangazwa katika sheria za mahakama hiyo.
Katika ripoti yake maalum kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, Francesca Albanese, ripota wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amezitaja hatua za Wazayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kuwa sawa na jinai za kimataifa na kusisitiza kwamba hatua za Tel Aviv zinahitaji kuchunguzwa haraka iwezekanavyo na Mahakamala ya Kimataifa ya Jinai.
Ombi la kutaka kuchunguzwa jinai za Israel linakuja wakati ambapo tokea mwaka 2021 Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imekuwa ikichunguza tuhuma za jinai za kivita na dhidi ya binadamu katika ardhi za Palestina hata hivyo, imeshindwa kutoa maamuzi yoyote kutokana na mashinikizo ya nchi za Magharibi. Kwa hakika Washington mara kwa mara imekuwa ikifunika jinai za Tel Aviv dhidi ya Wapalestina, na kuzuia kupitishwa maazimio dhidi ya utawala huo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na kuweka vizuizi katika mwenendo wa uchunguzi wa mahakama hiyo. Kuhusiana na hilo, tunaweza kutaja kesi ya mauaji ya mwandishi wa Al Jazeera Shirin Abu Aqleh, ambayo Marekani ilizuia kupelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Hii ni katika hali ambayo kuhusu vita vya Russia na Ukraine, Wamarekani wameomba mara kwa mara kufanyika vikao vya mahakama ya uhalifu wa kivita ili kushughulikia mashtaka yanayotolewa dhidi jeshi la Russia.
Hujuma za utawala ghasibu wa Kizayuni huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan zimeingia katika siku ya 44, ambapo mashirika ya kimataifa yanatahadharisha kuhusu kutokea mgogoro wa kibinadamu katika ardhi za Palestina, lakini vikosi vamizi vya Kizayuni kwa kupuuza maonyo hayo vinaendelea kuharibu hospitali na kuwaua kwa umati wagonjwa pamoja na wafanyakazi wa huduma za afya na matibabu pamoja na wakimbizi.