Bunge la Israel kujadili rasimu ya sheria ya kuwanyonga wafungwa Wapalestina
Waziri mwenye misimamo mikali na ya chuki katika baraza la mawaziri la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel amesema, bunge la utawala huo Knesset limepanga kujadili rasimu ya sheria yenye utata ya "kuwanyonga wafungwa wa Kipalestina".
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, gazeti la Kizayuni la Ma'ariv limeandika kuwa, Knesset leo Jumatatu itajadili hatua za utangulizi za kuwasilisha kwa mara ya kwanza sheria ya hukumu ya kifo kwa wafungwa wa Kipalestina.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel, Itamar Ben Gower, amesema chama anachokiongoza cha Nguvu ya Kiyahudi (Jewish Power) kimewasilisha rasimu hiyo ya kunyongwa wafungwa wa Kipalestina na kuongeza kuwa wanatarajia, rasimu hiyo itaungwa mkono na wajumbe wote wa Knesset.
Kwa mujibu wa duru za Palestina, utawala wa Kizayuni unawashikilia katika magereza yake Wapalestina zaidi ya elfu tano wakiwemo wanawake na watoto wadogo.
Utawala wa Kizayuni ulifuta hukumu ya kifo mwaka 1954, lakini mwezi Machi mwaka huu Knesset iliidhinisha kuwasilishwa katika hatua ya utangulizi rasimu ya sheria ambayo itawezesha kurejeshwa kwa hukumu ya kifo kwa "wafungwa wa Kipalestina waliopatikana na hatia ya kuwaua Waisraeli."
Ben Gower aliwasilisha rasimu hiyo ambayo iliungwa mkono na waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu, na kukabiliwa na wimbi la upinzani kutoka kwa Wapalestina.
Katika miaka ya karibuni, sheria ya hukumu ya kifo imependekezwa zaidi ya mara moja katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel), lakini Knesset imekataa kuidhinisha. Rasimu ya sheria hiyo lazima isomwe na kuidhinishwa bungeni mara tatu ili iweze kutekelezeka.
Kwa mujibu wa tovuti ya Middle East Monitor, harakati ya Hamas ilipendekeza makubaliano mapana na jumuishi ya kubadilishana mateka, ambapo kwa upande wake itawaachilia Wazayuni wote 240 inaowashikilia tangu tarehe 7 Oktoba, ili mkabala wake, utawala wa Kizayuni uwaachie huru wafungwa wote wa Kipalestina; hata hivyo Israel imetangaza kuwa itawakomboa mateka wake kwa kushadidisha operesheni za kijeshi katika Ukanda wa Gaza.../