Wayemen wafanya maandamano kulaani jinai za Wazayuni Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106024-wayemen_wafanya_maandamano_kulaani_jinai_za_wazayuni_gaza
Wananchi wa Yemen kwa mara nyingine tena wamefanya maandamano makubwa ya kulaani jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, na vile vile kuonyesha mshikamano wao na taifa la Palestina.
(last modified 2023-12-15T06:47:56+00:00 )
Dec 15, 2023 06:47 UTC
  • Wayemen wafanya maandamano kulaani jinai za Wazayuni Gaza

Wananchi wa Yemen kwa mara nyingine tena wamefanya maandamano makubwa ya kulaani jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, na vile vile kuonyesha mshikamano wao na taifa la Palestina.

Kwa mujibu wa Press TV, maandamano hayo yameshuhudiwa katika miji mbalimbali ya Yemen, ukiwemo mji mkuu Sana'a.

Wananchi wa Yemen walioshiriki katika maandamano hayo walikuwa wamebeba bendera za Yemen na Palestina, na mabango yenye jumbe za kulaani jinai za Israel na washirikia wake huko Gaza.

Wananchi wa Yemen walioshiriki maandamano hayo ya leo Ijumaa wametoa wito wa kusitishwa vita vya maangamizi ya umati vya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Raia wa kawaida Yemen wameendeleza maandamano yao ya kulaani jinai za Israel huko Gaza, huku jeshi la nchi hiyo ya Kiarabu likiendelea kufanya mashambulizi dhidi ya ngome za Wazayuni kwa kutumia ndege zisizo na rubani (droni), makombora na kusimamisha meli za Wazayuni katika Bahari Nyekundu.

Katika hatua nyingine, waungaji mkono wa Palestina nchini Marekani jana usiku walifanya maandamano ya kulaani jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Waandamanaji hao mjini Philadelphia, Pennsylvania walifunga barabara kuu na kusababisha msongamano mkubwa wa magari wakati wa maandamano hayo, ambapo mbali na kuonyesha mshikamano wao na Wapalestina, lakini pia wamesisitizia haja ya kusimamisha mapigano mara moja huko Gaza.

Jana usiku pia, wafuasi wa asasi ya kiraia ya Jewish Voice for Peace walifanya maanamano na kufunga barabara katika miji ya Washington, Boston, Atlanta, Chicago, Minneapolis, Seattle na Portland, Oregon.

Rais Joe Biden wa Marekani anakabiliwa na wito unaoongezeka wa kuunga mkono usitishaji vita Gaza.

Hapo jana pia, wafanyakazi wa utawala wa Biden waliandamana mbele ya Ikulu ya White House, wakitoa wito wa kusitishwa vita vya maangamizi ya umati vya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Kadhalika mwezi uliopita, zaidi ya wafanyakazi 800 wa serikali ya kitaifa na majimbo Marekani walitia saini barua, wakitaka msaada wa haraka wa Biden kwa usitishaji wa mapigano na usimamishaji wa haraka wa ghasia huko Gaza.