Baghdad: Mashambulizi ya US yamekiuka mamlaka ya kujitawala Iraq
(last modified Wed, 27 Dec 2023 02:53:26 GMT )
Dec 27, 2023 02:53 UTC
  • Baghdad: Mashambulizi ya US yamekiuka mamlaka ya kujitawala Iraq

Serikali ya Baghdad imelaani vikali mashambulizi dhidi ya kambi tatu za Harakati ya Kataib Hizbullah nchini Iraq yaliyofanywa na vikosi vamizi vya Marekani kwa amri ya Rais Joe Biden na kueleza kuwa, hujuma hizo hazikubaliki na zimekiuka mamlaka ya kujitawala Iraq.

Katika taarifa ya jana Jumanne, serikali ya Baghdad imeyataja mashambulizi hayo ya Marekani kama vitendo vya wazi vya uhasama ambavyo vitakuwa na taathira hasi kwa uhusiano wa pande mbili wa nchi mbili hizo.

Vikosi vamizi vya Marekani jana asubuhi vilikiuka mamlaka ya kujitawala Iraq na kushambulia kambi kadhaa za wapiganaji wa Harakati ya Hashd al Shaabi huko katikati ya mkoa wa Babel, kusini mwa Baghdad.

Watu 18 wakiwemo askari jeshi na wapiganaji wa Harakati ya Hashd al Shaabi wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo ya ndege za kivita za Marekani katika mji wa Al Hala katikati ya mkoa wa Babel.

Duru za kiusalama zimeiambia kanali ya televisheni al-Sumaria inayorusha matangazo yake kwa lugha ya Kiarabu kuwa, mwanachama wa Kataib Hizbullah ambayo ni sehemu ya Harakati ya Hashd al Shaabi ameuawa shahidi katika hujuma hizo.

Wanajihadi wa Kataib Hizbullah ya Iraq

Mashambulizi hayo ya wavamizi yanakuja huku kukiwa na ongezeko la chuki dhidi ya Marekani katika eneo lote la Asia Magharibi kutokana na  uungaji mkono wa Washington kwa Israel.

Kundi la Mapambano ya Kiislmu la Iraq, ambalo linaleta pamoja makundi kadhaa yanayoipinga Marekani, katika wiki za  karibuni limelenga vituo kadhaa vya jeshi vamizi la Marekani huko Iraq na Syria kutokana na hatua ya Washington ya kuunga mkono kwa hali na mali mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala katili wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Tags