Maelfu ya watoto wanaugua nimonia nchini Pakistan
Maafisa husika wa Afya wameripoti kutoka Pakistan kuwa watoto zaidi ya 19,000 katika jimbo la Punjab kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wamegunduliwa kuugua maradhi ya homa ya mapafu yaani nimonia (Pneumonia) baada ya kufanyiwa vipimo katika kipindi cha mwezi mmoja wa karibuni.
Maafisa hao wameeleza kuwa watoto wengi wanaugua nimonia kwa sababu ya hali ya hewa ya baridi, moshi na vumbi. Jamal Nasir Afisa wa Ngazi ya Juu wa Afya katika jimbo la Punjab huko Pakistan ameeleza kuwa ugonjwa huu wa nimonia unawaathiri watoto na hata watu wazima jimboni humo kila mwaka. Amesema, kila mwaka watoto 55,000 hadi 60,000 hupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo huko Pakistan; na hii si mara ya kwanza kushuhudiwa idadi kubwa kama hii ya vifo vya watoto vinavyosababishwa na nimonia huko Pakistan.
Jamal Nasir amewahimiza wazazi kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya kwa ajili ya kupatiwa chanjo ya kujikinga na nimonia. Amesema, chanjo dhidi ya nimonia inatolewa katika jimbo zima la Punjab na kwamba wazazi wanapasa kuhakikisha kuwa watoto wao wamepatiwa chanjo ya ugonjwa huo.
Pakistan imeakubwa na wimbi la baridi kali huku sehemu za kati na kaskazini mwa nchi hiyo zikishuhudia mvua na theluji kubwa hivi karibuni. Inafaa kuashiria hapa kuwa neumonia (Pneumonia) ni maambukizi kwenye mapafu. Mara nyingi ugonjwa huu husababishwa na bakteria au virusi. Ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa kupumua.
Watoto lakini pia watu wazima wanaweza kuugua ugonjwa huu. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Watoto 740,000 walio na umri wa chini ya miaka mitano wamefariki dunia kutokana na homa hiyo ya mapafu mwaka 2019. Kila inapowadia tarehe 12 Novemba nchi mbalimbali duniani huadhimisha "Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Pneumonia".