Wabahrain waendesha kampeni ya uasi wa kiraia
Wananchi wa Bahrain leo wameandamana katika miji na vijiji kadhaa katika kampeni ya uasi wa kiraia huku wakijitayarisha kuadhimisha mwaka wa tano wa mwamko dhidi ya utawala wa kiimla wa Aal Khalifa.
Ripoti zinasema maduka yalifungwa huku wafanyabishara wakianzisha mgomo wa siku mbili kabla ya Februari 14 ambayo ni siku ya kuanza mwamko wa Kiislamu nchini humo mwaka 2011. Watu kadhaa wameuawa katika maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika nchini humo takribani kila siku kwa muda wa miaka mitano sasa huku mamia ya watetezi wa haki za binadamu na viongozi wa upinzani wakifungwa jela.
Utawala wa kifalme wa Manama umekuwa ukipata misaada ya kijeshi kutoka nchi za Magharibi na Saudi Arabia katika kuwakandamiza wananchi wanaoshiriki maandamano ya amani. Mkuu wa Usalama Bahrain Tariq al Hussein amesema uasi wa kiraia ni kosa na kwamba wanaoshiriki wataadhibiwa. Wananchi wa Bahrain wamesisitiza kuwa wataendeleza maandamano yao hadi pale utawala utakaposikiliza matakwa yao ambayo ni pamoja na kumalizwa ubaguzi, kufanyika marekebisho katika mfumo wa utawala na kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa.