NATO yatafakari kuingia vitani Syria, Iraq
Shirika la Kijeshi la NATO linatafakari kuingia katika vita vinavyoendelea katika nchi za Syria na Iraq.
Hayo yamedokezwa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Ashton Carter ambaye amedai kuwa NATO itaingia katika vita kwa lengo la kukabiliana na magaidi wa ISIS katika nchi hizo mbili.
Akizungumza Alhamisi baada ya kukutana na nchi wanachama wa NATO mjini Brussels, Carter alisema Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg anatafakari namna shirika hilo la kijeshi linaweza kuingia vitani Syria na Iraq. Hivi sasa wanachama wote 28 wa NATO wamejiunga na muungano unaoongozwa na Marekani katika vita vya Syria tokea 2014. Hata hivyo NATO kama taasisi haijaingia katika vita hivyo.
Hayo yanajiri kaika hali ambayo Alhamisi Waziri Mkuu wa Russia Dmitry Medvedev alionya kuwa iwapo vikosi vya kigeni vitavamia Syria basi huo utakuwa mwanzo wa vita vipya vikuu vya dunia.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria Walid al Muallem naye ameonya kuwa askari wowote vamizi Syria watarejea nyumbani kwao katika majeneza. Saudi Arabia ilitangaza hivi karibuni kuwa inatafakari kutuma askari wa nchi kavu Syria.
Marekani na waitifaki wake wanaipinga vikali serikali halali ya Syria huku wakiunga mkono magaidi na wanamgambo wanaotaka kuipindua serikali ya Rais Bashar al Assad.