Jun 16, 2024 07:26 UTC
  • Je, utawala wa Israel utaangukia kwenye mtego wa Hizbullah ya Lebanon au la?

Kufuatia kuongezeka minong'ono ya vyombo vya habari na kisiasa kuhusu uwezekano wa jeshi la utawala haramu wa Israel kuanzisha mashambulizi ya pande zote kusini mwa Lebanon, uvumi umeenea kuwa Hizbullah imejiandaa vilivyo kutoa pigo kali la kulipiza kisasi dhidi ya utawala huo wa kigaidi iwapo utafanya mashambilizi hayo.

Falsafa ya kuundwa Hizbullah ya Lebanon ilikuwa ni kuyatimua majeshi ya Kizayuni yanayoikalia kwa mabavu ardhi ya Lebanon na kuzuia Israel kuivamia tena nchi hiyo ya Kiarabu.

Mgogoro na vita kati ya Hizbullah na Israel vinarejea nyuma mwanzoni mwa miaka ya 1980, wakati Hizbullah ilipoasisiwa. Vita vya miaka ya 2000 na 2006 kati ya Hizbullah na Israel viliandaa fursa ya kurudishwa nyuma majeshi ya Kizayuni, mafanikio ya kihistoria ambayo yaliimarishwa na azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kufuatia operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, wajuzi wa mambo wamekuwa wakizungumzia uwezekano wa kuzuka vita vipya kati ya Hizbullah na Israel baada ya kupita miaka 17. Licha ya baadhi ya juhudi za kidiplomasia zinazofanywa na Marekani, Ufaransa na Qatar kwa ajili ya kuzuia kutokea vita vya aina hiyo, lakini inaonekana kuwa mivutano kati ya Hizbullah na utawala ghasibu wa Israel imefikia kiwango kipya ambapo  kuna uwezekano wa utawala huo katili kuvamia kusini mwa Lebanon wakati wowote.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyochapishwa karibuni na Hizbullah, idadi ya askari wa harakati hiyo inakadiriwa kuwa karibu askari laki moja. Hata hivyo baadhi ya vyanzo vya Magharibi vimetangaza idadi ya askari hao kuwa ni 50,000 ambapo askari hai wanaohudumu jeshini ni 30,000 na vikosi vya akiba ni 20,000.

Sky News imetangaza katika ripoti kwamba idadi ya makombora ya Hizbullah inafikia 100,000, lakini vyanzo vingine vinasema idadi hiyo ni makombora 150 hadi 200.

Kurushwa kwa wakati mmoja makombora ya Hizbullah ya Lebanon kunaweza kulenga na kuharibu kabisa miundombinu muhimu ya utawala haramu wa Israel, kama vile matangi ya kuhifadhia amonia katika bandari ya Haifa. Silaha nyingine ya kimkakati ya Hizbullah katika vita na jeshi la Israel ni ndege zake zisizo na rubani, ambazo zinaweza kuvuruga utendaji wa mfumo wa ulinzi wa anga wa Iron Dome na hatimaye kulenga na kuuharibu kabisa mfumo huo.

Mashambulio ya karibuni ya Hizbullah dhidi ya utawala ghasibu wa Israel

Siku chache zilizopita, picha za kulengwa mfumo wa Iron Dome wa utawala wa Israel na makombora ya "Almasi", ambalo ni moja ya makombora mapya ya kushtukiza ya muqawama wa Lebanon dhidi ya mifumo ya ulinzi wa anga ya Wazayuni, zilionyeshwa kwenye vyombo ya habari duniani.

Makombora ya kulenga vifaru na meli ni jinamizi jingine kwa Wazayuni katika vita vinavyoweza kutokea wakati wowote kati yao na Hizbullah ya Lebanon, jambo ambalo linaweza kufufua kumbukumbu chungu za vita vya siku 33 kwa utawala wa Israel.

Harakati ya Hizbullah, pia ina mtandao mkubwa wa ngome, njia za chini kwa chini na mahandaki kwenye mpaka wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel, jambo ambalo linaweza kuishtukiza Israel katika maeneo tofauti ya mpaka huo. Njia hizo za siri za chini ya ardhi bila shaka zinawawezesha wapiganaji wa Hizbullah kutumia walengashabaha, makombora na droni nyepesi kulenga kirahisi vifaru na magari ya deraya ya utawala wa Israel. Uwezo mwingine wa mtandao huo wa siri wa njia za chini kwa chini ni kuwa unawawezesha askari wa Hizbullah kupenya hadi ndani kabisa ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Kwa kutumia mazingira asili ya eneo la kaskazini mwa Palestina, vikosi vya Hizbullah vinaweza kuushambulia kirahisi utawala huo kuliko ilivyokuwa miaka 17 iliyopita.

Kwa kuzingatia mfululizo wa matukio ya baada ya tarehe 7 Oktoba mwaka jana, kuna uwezekano kwamba Israel imechagua kuanzisha vita vya pande zote na Hizbullah badala ya kutegemea mazungumzo ya kidiplomasia, ili kurudisha usalama kwenye mipaka ya kaskazini na kutaka kuidhoofisha harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu.

Kwa vyo vyote vile kwa sasa tunapaswa kusubiri na kuona iwapo Netanyahu atakubali hatari ya kuishambulia Lebanon au atafadhilisha siasa za kudhibiti mivutano katika eneo.