Jun 17, 2024 06:33 UTC
  • Ripoti: ICC kutoa waranti wa kukamatwa Netanyahu karibuni

Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), katika kipindi cha siku 10 zijazo huenda ikafikia uamuzi wa kutolewa waranti wa kumtia nguvuni Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, kanali ya 13 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imeripoti kuwa, kuna wasiwasi ndani ya Israel kuhusu uwezekano wa Mahakama ya ICC kutoa waranti wa kimataifa wa kukamatwa maafisa wakuu wa Israel akiwemo Netanyahu, na waziri wa vita wa utawala huo, Yoav Gallant.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa, wataalamu waandamizi wa kisheria katika wizara ya mambo ya nje ya utawala haramu wa Israel wanahaha na kufanya vikao virefu na vya mara kwa mara vya kujadili uwezekano wa kutolewa waranti dhidi ya Netanyahu.

Nchi nyingi duniani, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Afrika Kusini, Colombia na hata Palestina yenyewe, zimekuwa zikiishinikiza mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi imkamate Netanyahu kwa kuhusika na jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza.

Mahakama ya ICC

Hata hivyo, viongozi mbali mbali wa Marekani akiwemo Rais Joe Biden wamekosoa vikali ombi la Karim Khan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC) la kutaka kutolewa waranti dhidi ya Netanyahu.

Viongozi wa Marekani wanaendeleza kampeni kubwa ya kuzuia hatua yoyote ya mahakama hiyo ya kimataifa kutoa kibali cha kukamatwa viongozi watenda jinai na mauaji ya kimbari wa Israel, hususan Netanyahu.

Zaidi ya Wapalestina 37,000, wakiwemo watoto zaidi ya 15,500 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 7, 2023, na karibu asilimia 70 ya miundombinu ya kiraia ya Ukanda huo uliozingirwa imeharibiwa.

Tags