HAMAS: Kuendelea kutambuliwa Palestina kutahitimisha unazi wa Kizayuni
(last modified Sat, 22 Jun 2024 11:19:32 GMT )
Jun 22, 2024 11:19 UTC
  • HAMAS: Kuendelea kutambuliwa Palestina kutahitimisha unazi wa Kizayuni

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS sanjari na kukaribisha kwa mikono miwili na kupongeza hatua ya Armenia ya kulitambua rasmi taifa huru la Palestina, imesisitiza kuwa mwenendo huo wa mataifa ya dunia kuitambua Palestina kama nchi huru utapelekea kufikia ukingoni unazi wa Kizayuni.

Taarifa ya HAMAS imesema kuwa, kitendo cha Armenia cha kulitambua rasmi taifa huru la Palestina ni hatua moja mbele na muhimu katika njia ya kutambuliwa haki za msingi za Wapalestina na jamii ya kimataifa.

Harakati hiyo inayopigania ukombozi wa Palestina imesisitiza kuwa, kitendo cha Armenia na nchi nyinigine dunia kuitambua Palestina kitaharakisha mchakato wa kuanzishwa nchi huru ya Palestina, mji mku wake ukiwa Quds.

HAMAS imetoa mwito kwa mataifa yote ya dunia kuutenga, kuususia na kuvunja uhusiano wao na utawala huo ghasibu unaofanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza tokea Oktoba 7, 2023.

Kundi hilo la muqawama la Palestina limesema, mataifa yote ambayo yanapinga vita vya mauaji ya halaiki vya utawala wa Israel dhidi ya Gaza, yanapaswa kuitambua rasmi Palestina likisisitiza kuwa, kutambuliwa nchi hiyo ni haki ya kisheria ya taifa hilo madhulumu.

Maandamano ya kuiunga mkono Palestina yanaendelea kufanyika katika kona zote dunia

Jana Ijumaa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Armenia ilitangaza kuwa inalitambua rasmi taifa huru la Palestina, na hivyo kukaidi matakwa ya utawala haramu wa Israel ambao unapingana na hatua kama hizo.

Uhispania, Norway na Ireland tayari zilishatangaza uamuzi wa kuitambua rasmi Palestina mnamo Mei 28 na hivyo kufanya idadi ya nchi zilizoitambua nchi huru ya Palestina hadi sasa kukaribia 150. Aidha mapema mwezi huu, Bunge la Taifa la Slovenia lilipiga kura kuunga mkono kubariki azma ya taifa hilo ya kuitambua Palestina kama nchi huru. 

Tags