Hamas: Al Dhaif yuko salama, anaendeleza vita dhidi ya Wazayuni huko Gaza
(last modified Sun, 14 Jul 2024 12:08:58 GMT )
Jul 14, 2024 12:08 UTC
  •  Mohammed Dhaif yuko
    Mohammed Dhaif yuko

Afisa mwandanizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) anasema kamanda wa tawi la kijeshi wa harakati hiyo Mohammed Dhaif yuko "salama" licha ya madai ya Israel ya kutaka kumuua katika shambulio dhidi ya kambi ya al-Mawasi kusini mwa Gaza.

"Kamanda Mohammed Dhaif yuko salama na anasimamia moja kwa moja" operesheni za kijeshi dhidi ya vikosi vya jeshi la Israeli," afisa wa Hamas ambaye hakutajwa jina ameliambia shirika la habari la AFP leo Jumapili.

Jana Jumamosi, jeshi la Israel lilishambulia eneo lililotangazwa kuwa usalama katika kambi ya al-Mawasi kusini mwa Gaza, na kuua Wapalestina wasiopungua 100 na kujeruhi wengine 300. Shambulio hilo lilikuwa baya zaidi la Israel katika Gaza katika kipindi cha wiki kadhaa za karibuni.

Gaza

Israel ilidai kuwa shabaha ya shambulio hilo huko al-Mawasi alikuwa Mohammed Dhaif, ingawa waziri mkuu wa utawala huo katili, Benjamin Netanyahu alisema hana uhakika kama kamanda wa Hamas ameuawa.

Hamas imepinga madai hayyo ya Israel kwamba ilimlenga Mohammed Dhaif ikiyataja kuwa ni "uongo", na kusema "raia wasio na ulinzi" ndio waliolengwa katika shambulio hilo la anga.

Mohammed Dhaif ni miongoni mwa waanzilishi wa tawi la kijeshi la Hamas, Qassam Brigades, katika miaka ya 1990 na anaongoza kikosi hicho kwa zaidi ya miaka 20.

Dhaif hajaonekana hadharani kwa miaka mingi, na picha zake chache zinapatikana mtandaoni.