Aug 08, 2024 02:23 UTC
  • Kiwewe cha Wazayuni baada ya kuchaguliwa Yahya Sinwar kuwa mkuu mpya wa ofisi ya kisiasa ya HAMAS

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imemteua Yahya Sinwar kuwa Kiongozi wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati hiyo ya muqawama, kujaza nafasi iliyoachwa wazi na hayati Ismail Haniyah.

Shahidi Haniyah aliuawa kigaidi na utawala wa Kizayuni hapa mjini Tehran tarehe 31 Julai, siku moja baada ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian.

Kuchaguliwa Yahya Sinwar kuwa mkuu mpya wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) kumeibua mshangao, hofu na wahaka mkubwa kwa utawala wa Kizayuni.

Yahya Ebrahim Sinwar ndiye mwanzilishi wa idara ya usalama ya Hamas, iliyopewa jina la "Majd", inayoshughulikia kesi za usalama wa ndani. Utawala wa Kizayuni ulifeli katika shambulio la kigaidi la kutaka kumuua Sinwar.

Kuchaguliwa Yahya Sinwar kuwa mkuu mpya wa ofisi ya kisiasa ya Hamas kumepokewa kwa hisia mbalimbali katika eneo na dunia, na baadhi wameuchukulia uteuzi huu kuwa ni wa kuimarisha muqawama na kuendeleza njia ya shahidi Ismail Haniyeh.

Shirika la Utangazaji la Israel limesema kuwa, uteuzi wa Sinwar unashangaza na ni ujumbe kwa Israel kwamba yu hai na kwamba uongozi wa Hamas huko Gaza uko imara, upo na utabakia.

Yahya Sinwar, kiongozi mpya wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS

 

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati wa gazeti la Times of Israel, Avi Iskharov, amesema kuwa harakati ya Hamas imechagua "mtu hatari zaidi kuiongoza," hasa kwa vile Israel inamtambua Sinwar kuwa mhandisi wa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa Oktoba 7 mwaka jana (2023), ambayo ilitoa kipigo kikubwa kwa jeshi la utawala huo, na kuchafua taswira ya idara zake za kijasusi na kiusalama mbele ya macho ya walimwengu.

Kwa upande wake televisheni rasmi ya Israel, Kan, imesema kuwa uteuzi wa Sinwar kushika nafasi ya Ismail Haniyeh unaonyesha kuwa Hamas bado ina nguvu na ni imara huko Gaza.

Yahya Sinwar aliachiwa huru pamoja na Wapalestina wengine 1,000 mwaka 2011, katika mabadilishano baina ya mateka wa Kipalestina na wanajeshi wa Israel, baada ya kuwa gerezani kwa miaka 22.

Baada ya kutoka gerezani, Sinwar alichaguliwa kuwa mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas wakati wa uchaguzi wa ndani wa harakati hiyo mwaka 2012. Pia alichukua uongozi wa tawi la kijeshi la Hamas, Brigedi za Izzuddin al-Qassam na kupewa jukumu la uratibu kati ya Ofisi ya Kisiasa ya harakati hiyo na uongozi wa tawi lake la kijeshi.

Osama Hamdan, mmoja wa wanachama waandamizi wa Hamas amesema kuhusiana na suala hili kwamba: Kuchaguliwa haraka Sinwar kuwa mkuu mpya wa ofisi ya kisiasa kwa kauli moja kunaonyesha nguvu na uimara wa Hamas.

Shahidi Ismail Hania

 

Hamdan amesisitiza kuwa: "Ujumbe wa Hamas ni kwamba imemchagua kuwa kiongozi wake mtu ambaye amekuwa mtunza amana katika jihadi na mapambano katika medani ya vita huko Gaza kwa zaidi ya siku 300."

Yahya Sinwar amechaguliwa kuwa mkuu mpya wa ofisi ya kisiasa ya Hamas katika hali ambayo bado anaishi Gaza licha ya hujuma na vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda huo.

Hatua ya Hamas ya kumteua Sinwar inaonesha kuwa, makundi ya muqawama ya Palestina bado yanaona kuwa, muqawama na kusimama kidete dhidi ya Wazayuni ndio chaguo lao kuu la kufikia malengo ya kistratijia na kisiasa.

Mkuu huyo mpya wa ofisi ya kisiasa ya Hamas ana historia ndefu ya mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni, na pia anatajwa kuwa mbunifu na kiongozi wa operesheni ya "Kimbunga cha Al-Aqswa ".

Mwenendo wa matukio ya vita vya Gaza umeleta uthabiti na mshikamano zaidi kati ya makundi ya wapiganaji wa Palestina. Katika hali hiyo, kuchaguliwa Yahya Sinwar kutapelekea mshikamano na ushirikiano zaidi wa makundi ya muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni.