Hizbullah yashambulia kwa mafanikio kambi ya jeshi la Israel huko Giaton
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kwamba imeshambulia kwa mafanikio kambi muhimu ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo ya kaskazini yanayokaliwa kwa mabavu.
Hizbullah imesema katika taarifa mapema leo Jumatatu kwamba maroketi ya Katyusha yalivurumishwa kuelekea katika makao makuu mapya ya Idara ya 146 ya jeshi la Israel huko Giaton.
Hali kadhalika taarifa hiyo imebaini kuwa operesheni hiyo imetekelezwa kujibu mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel kwenye maeneo ya raia kusini mwa Lebanon, hasa katika mji wa Maaroub.
Kwa mujibu wa Hizbullah shambulio hilo la roketi pia lililenga kuonyesha uungaji mkono wa harakati hiyo ya Lebanon kwa Wapalestina huko Gaza ambao wanakabiliwa na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na Israel..
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya utawala wa Israel, mfumo wa ulinzi wa anga wa Iron Dome au Kuba la Chuma wa Israel haukuweza kuzuia makombora mengi ya Hizbullah.
Utawala wa Israel umekuwa ukifanya mashambulizi ya karibu kila siku dhidi ya maeneo ya kusini mwa Lebanon tangu Oktoba 7, wakati ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza.
Hizbullah pia imeahidi kulipiza kisasi cha damu ya Fuad Shukr, mmoja wa makamanda wakuu wa kundi hilo, na Ismail Haniyeh, aliyekuwa kiongozi kisiasa wa harakati ya Kiislamu ya kupigania ukombozi wa Palestina, Hamas, ambao waliuawa katika operesheni tofauti za mauaji zilizofanywa na Tel Aviv katika mji mkuu wa Lebanon Beirut na mji mkuu wa Iran, Tehran, mwishoni mwa mwezi uliopita.
Akizungumza siku ya Jumanne, Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyed Hassan Nasrallah alisema utawala ghasibu wa Israel hauwezi kujilinda na unaiogopa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na jibu la muqawama dhidi ya mauaji hayo.