Aug 26, 2024 11:26 UTC
  • Wananchi wa Uturuki wafanya maandamano Istanbul kuunga mkono Gaza

Kwa mara nyingine tena, wananchi wa Uturuki wamefanya maandamano ya kulalamikia siasa za kijeshi na mauaji yanayofanywa na utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya wanawake na watoto wadogo katika eneo la Ukanda wa Gaza linalokaliwa kwa mabavu.

Wilaya ya Fatih mjini Istanbul jana Jumapili ilishuhudia maandamano makubwa ya kulaani vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uturuki, maandamano hayo yalianza katika Msikiti wa kihistoria wa Fatih mjini Istanbul na kumalizika kwa kushirikisha takriban watu elfu tatu katika wilaya ya Edirne.

Washiriki wa maandamano hayo walibeba bendera za Uturuki na Palestina na na mabango yenye jumbe za kuunga mkono Palestina na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Gaza.

Mkuu wa Jumuiya ya Uhuru na Mshikamano ya Mavi Marmara, Beheşti Ismail Songür amesema kuwa, taswira ambayo utawala wa Israel unaweka kwenye vyombo vya habari kuhusiana na uwezekano wa kuingia Gaza si ya kweli.

Jinai za utawala katili wa Israel Gaza

Amesema Msafara wa Uhuru uliokuwa ukijiandaa kuondoka Istanbul kwenda kutoa misaada kwa watu wa Gaza, umekabiliwa na vikwazo vingi kutoka kwa utawala wa Kizayuni.

Waandamanaji hao pia wamezitaka jumuiya za kimataifa kusitisha mashambulizi ya Israel dhidi ya raia wa Palestina. Walikuwa wamebeba mabango yaliyoandikwa "Free  Palestine". Waandamanaji hao walikuwa wakitoa nara za "Mauti  kwa Israeli na mshirika wake Marekani".  

Mapema mwezi huu, Uturuki ilitangaza kuwa, imewasilisha rasmi ombi la kujiunga na kesi ya Afrika Kusini iliyowasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ).

Tags