Sep 08, 2024 04:22 UTC
  • Matokeo ya vita vya Gaza kwa walowezi wa Kizayuni

Mbali na kuwa utawala wa Kizayuni haujafikia malengo yake yoyote ya kijeshi katika vita vya Gaza, unakabiliwa pia na ongezeko la changamoto za walowezi wa Kizayuni.

Vita vya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza vimeingia katika mwezi wake wa kumi na mbili. Vita hivyo vinakaribia kukamilisha mwaka mmoja, katika hali ambayo matokeo yake kwa walowezi wa Kizayuni yanaendelea kudhihirika wazi zaidi. Changamoto za walowezi katika maeneo ya kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni nyingi kuliko maeneo mengine kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Hizbullah ya Lebanon. Kuendelea mashambulizi ya Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon katika eneo la kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu kumeongeza idadi ya Wazayuni wanaotafuta msaada wa matibabu ya kisaikolojia. Kwa mujibu wa gazeti la Israel la Yediot Aharnot, Ethan Davidi, mkuu wa baraza la walowezi wa Kizayuni wa eneo la Margliot anasema kuwa Hizbullah imekuwa ikifuatilia na kuweka chini ya uangalizi wake vitongoji vya walowezi wa eneo hilo kwa muda mrefu na sasa imevigeuza kuwa magofu kupitia mashambulizi yake ya mara kwa mara. Hali hii imewasababishia hasara kubwa ya kisaikolojia walowezi katika maeneo ya kaskazini.

Aidha tangu kuanza operesheni ya Hizbollah kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu, idadi kubwa ya walowezi wa Kizayuni katika eneo hilo wamelazimika kuhama makazi yao. Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, zaidi ya walowezi laki mbili wa Kizayuni wamelazimika kuyahama makazi yao kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Kwa mujibu wa Jumuiya ya Ulinzi na Usalama ya utawala wa Kizayuni, takriban makombora 8,000 yamevurumishwa na Hizbullah kuelekea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. Zaidi ya nyumba na majengo elfu moja yameharibiwa na zaidi ya hekari 2,520 za ardhi zimeteketezwa moto. Isitoshe, tofauti kubwa za kiusalama zinazotekelezwa kati ya walowezi wa kaskazini na walowezi wa maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu zimeibua mfadhaiko mkubwa kwa walowezi wa maeneo ya kaskazini kiasi cha kuwafanywa wahisi kuwa wamepuuzwa na kutengwa na serikali ya Tel Aviv.

Maandamano ya Wazayuni dhidi ya serikali ya Netanyahu

Baada ya takriban mwaka mmoja wa vita, wakimbizi wa Kizayuni bado hawajui nini kinawasubiri na iwapo watarejea makwao au la. Kinachowaongezea msongo wa mawazo na mashinikizo ya kisaikolojia ni kwamba baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu bado halina mpango wa kumaliza vita wala wa kuwarejesha wakimbizi hao katika maeneo ya kaskazini. Kwa hakika wakimbizi wa Kizayuni wanakabiliwa na hali ngumu ambayo imewafanya wachanganyikiwe kifikra, hali ambayo ni mbaya zaidi kwa watoto wao.

Mameya watatu wa kaskazini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu walitangaza hivi karibuni katika taarifa ya pamoja kwamba watakata uhusiano na baraza la mawaziri la Israel hadi pale baraza hilo litakapowasilisha mpango wa kurejesha usalama katika eneo la kaskazini na kuwadhaminia walowezi usalama wao.

Kutokana na athari na madhara ya vita vya Gaza kwa walowezi hao hususan katika eneo la kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, maandamano ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya baraza la mawaziri la Netanyahu yameongezeka tena katika siku za karibuni, ambapo waandamanaji wanataka kumalizika vita na kurejea maisha yao katika hali ya kawaiada. Maandamano ya kuhitimisha vita yameenea katika miji mingine ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hususan Tel Aviv ambapo mamia ya maelfu ya wakazi wa mji huo wanashiriki katika maandamano makubwa wakitaka vita hivyo visimamishwe mara moja.