Sep 08, 2024 06:45 UTC
  • Yemen yatungua ndege ya Marekani, yaapa kukabiliana na uwendawazimu wa Israel

Jeshi la Yemen limetungua ndege ya kivita ya Marekani isiyo na rubani huku waziri wa ulinzi wa nchi hiyo akiapa kuendeleza operesheni zinazoiunga mkono Palestina katika kupinga vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelea kufanywa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Ukanda wa Gaza.

Jeshi la Yemen limetungua kwa kombora ndege nyingine ya kisasa kabisa ya Marekani ikiwa ni hatua ya kuwaunga mkono Wapalestina wanaokabiliwa na mauaji ya kimbari ya Israel kwa himaya ya Marekani katika Ukanda wa Gaza. Aidha operehseni hiyo ni katika fremu ya kukabiliana na hujuma ya Marekani dhidi ya Yemen.

Msemaji wa Majeshi ya Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree alitangaza Jumamosi kwamba ndege ya kivita isiyo na rubani ya Marekani iliyolengwa ni aina ya MQ-9 Reaper yenye thamani ya karibu dola milioni 30. Hiyo ni ndege ya nane ya aina hiyo kutunguliwa na vikosi vya ulinzi vya Yemen.

Wakati huo huo Waziri wa Ulinzi Meja Jenerali Mohammed Nasser al-Atifi amesema haiwezekani kusitasita au kurudi nyuma kutoka kwenye msimamo wa Yemen wa kuunga mkono Gaza.

Akizungumza Jumamosi, ameongeza kuwa:"Bila shaka majibu yenye nguvu na ya kishindo ya Yemen kwa mfumo wa Kinazi wa Israel yanakuja, na tutakabiliana na uwendawazimu wa Kizayuni kwa nguvu za Yemen, ambazo wamezionja baharini."

Vikosi vya Wanajeshi vya Yemen vimekuwa vikiendesha mashambulizi mengi dhidi ya utawala haramu wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu tangu Oktoba 7, wakati utawala huo ulipoanzisha vita dhidi ya Gaza. Utawala haramu wa Israel hadi sasa umeua Wapalestina karibu 41,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Vikosi vya Yemen pia vimekuwa vikilenga meli za kibiashara zinazofungamana na utawala haramu wa Israel kama njia ya kujaribu kuulazimisha utawala huo usitishe mauaji ya kimbari na mzingiro dhidi ya Gaza.