Shambulio la Hizbullah laangamiza wanajeshi 14 wa Israel
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imeshambulia vituo viwili vya kijeshi vya utawala wa Israel kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani na kuua wanajeshi 14 wa utawala huo.
Taarifa iliyotolewa na Hizbullah imesema kuwa: Katika kuendeleza mapambano ya kulitetea taifa imara la Palestina eneo la Ukanda wa Gaza na kuunga mkono mapambano yake ya kishujaa, na kwa ajili ya kulinda ardhi ya Lebanon na taifa lake na kujibu mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya miji, vijiji na raia, wapiganaji wa Muqawama wa Kiislamu jana Jumatano walishambulia Kambi ya Amiad (kaskazini mwa Ziwa Tiberias) kwa makombora, na kulenga shabaha moja kwa moja.
Katika taarifa nyingine, Hizbullah imetangaza kuwa imeshambulia kambi ya Nafiyeh Zif ya utawala wa Kizayuni kwa kutumia ndege zisizo na rubani kupiga shabaha kwa usahihi.
Duru za Kizayuni zimekiri kupitia televisheni ya lugha ya Kiarabu ya Sky News kwamba askari 14 wa utawala wa Kizayuni wameuawa katika mapigano ya nchi kavu na wapiganaji wa Hizbullah katika eneo la mpaka wa kusini mwa Lebanon.