Walowezi wa Kizayuni wafanya uvamizi tena katika msikiti wa al-Aqswa
Walowezi wa Kizayuni kwa mara nyingine tena wamefanya uvamizi dhidi ya msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa huko Quds Tukufu Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Kwa mujibu wa duru za habari, walowezi wa Kizayuni jana Alkhamisi waliendelea tena na vitendo vyao vya kuuvunjia heshima msikiti mtakatifu wa al-Aqswa.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, walowezi hao wa Kizayuni wakisindikizwa na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel waliingia katika uwanja wa msikiti huo kupitia upande wa Bal al-Maghariba.
Kuingia katika eneo hilo takatifu walowezi hao kulipelekea kutokea mapigano kati yao na waumini waliokuwamo msikitini humo ambao walisikika wakipiga nara kupinga kuingia walowezi hao wa Kizayuni.
Hii sio mara ya kwanza kwa walowezi wa Kiyahudi kuuvamia msikiti huo mtakatifu ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kufanya vitendo vinavyokinzana kabisa na heshima na utukufu wa msikiti huo.
Hatua hizo za kuyavunjia heshima maeneo matakatifu huko Palestina zinakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hujuma hizo na ukandamizaji wa jeshi la Israel zimepelekea kutawanyika cheche za Intifadha mpya huko Palestina.
Itakumbukwa kuwa, tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za utawala wa Kizayuni. Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha ya Quds.