Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za muqawama wa Iraq dhidi ya utawala wa Kizayuni
Muqawama wa Kiislamu wa Iraq umelenga shabaha moja muhimu ya utawala habithi wa Kizayuni kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).
Muqawama wa Kiislamu wa Iraq umetangaza katika taarifa kuwa, ikiwa ni katika kukabiliana na mauaji na jinai za kinyama zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya raia wakiwemo watoto, wanawake na wazee, wanamapambano wa Kiislamu wa Iraq wameshambulia shabaha muhimu ya utawala huo katili kwa ndege isiyo na rubani mapema leo Jumatano asubuhi.
Taarifa hiyo pia inasisitiza kuendelea kwa oparesheni za kuponda ngome za adui mzayuni kwa mwelekeo huo huo unaoongezeka kila siku.
Kundi la Muqawama wa Kiislamu la Iraq pia lilitangaza katika taarifa siku ya Jumanne kwamba, lililenga shabaha tano za Wazayuni katikati na kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Wanamuqawama wa Iraq wamesema walifanya oparesheni hiyo kwa kutumia kombora la hali ya juu la cruise linalojulikana kama "Al-Aqrab" na ndege isiyo na rubani.
Tangu tarehe 7 Oktoba mwaka uliopita utawala wa Kizayuni umefanya kila aina ya jinai za kivita sambamba na mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina huko Ukanda wa Gaza na kuua Wapalestina wapatao 42,000 na kujeruhi wengine zaidi ya 97,000.
Utawala huo unaoua watoto haukuishia katika kufanya jinai za kutisha huko Gaza bali umeeneza jinai hizo kusini mwa Lebanon ambapo umeua zaidi ya raia 2,000 wa nchi hiyo. Mapambano ya muqawama katika nchi za Iraq, Lebanon na Yemen yamejibu vikali mashambulizi hayo ya Kizayuni na kusimama kidete na kwa ujasiri mkubwa dhidi ya utawala huo tangu kuanza mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza ili kumlazimisha adui huyo Mzayuni asitishe mashambulizi hayo haraka iwezekanavyo.