Israel imeua waandishi habari 188 wa Kipalestina tangu Oktoba mwaka jana
(last modified Sun, 10 Nov 2024 11:58:46 GMT )
Nov 10, 2024 11:58 UTC
  • Israel imeua waandishi habari 188 wa Kipalestina tangu Oktoba mwaka jana

Ofisi ya vyombo vya habari katika Ukanda wa Gaza, ambako utawala wa Israel umekuwa ukiendesha vita vya mauaji ya kimbari tangu Oktoba mwaka jana, inasema waandishi wa habari 188 wa Kipalestina wameuawa shahidi tangu kuanza kwa mashambulizi hayo ya kikatili ya kijeshi.

Ofisi hiyo litoa takwimu hiyo siku ya Jumamosi, ikiwataja wanahabari wanne kama waathiriwa wa hivi majuzi zaidi wa mashambulizi hayo.

Imewatambulisha wanne kuwa ni Zahraa Mohammad Abu Sukheil, Ahmad Mohammad Abu Sukheil, Mustafa Khadr Bahar, na Abdel Rahman Khadr Bahar.

Ofisi hiyo imesema "inalaani vikali hatua ya utawala haramu wa Israel ya kuwalenga na kuwaua  waandishi wa habari wa Kipalestina na kwamba utawala huo unabeba dhima ya uhalifu huo wa kutisha."

Aidha ofishi hiyo imetoa wito kwa jamii ya kimataifa, mashirika ya kimataifa, na wale wanaojihusisha na kazi ya uandishi wa habari duniani kote kuchukua hatua dhidi ya utawala wa Israel na kuushinikiza ukomeshe mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina sambamba na kuufikisha katika mahakama za kimataifa.

Ofisi ya vyombo vya habari katika Ukanda wa Gaza pia imesema utawala wa Israel na Marekani, kama mshirika mkubwa wa Israel, pamoja na nchi nyingine zinazosaidia mauaji ya kimbari zinahusika kikamilifu katika jinao za utawala huo ghasibu.

Takriban Wapalestina 43,552 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuawa na wengine 102,765 kujeruhiwa tangu Israel ianzeishe vita vya mauaji ya kimbari Gaza Oktoba 7 mwaka jana..