Putin ataka kuundwa nchi huru ya Palestina
Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza udharura wa kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Quds tukufu.
Katika ujumbe wake uliosomwa kwenye mkutano wa viongozi wa nchi za Kiarabu unaofanyika nchini Mauritania, Putin amesema kuwa, Moscow inaunga mkono suala la kuanza tena mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati yatakayopelekea kuundwa nchi huru ya Palestina ambayo mji mkuu wake utakuwa Quds. Rais wa Russia amesema kuwa, hali ya sasa ya Palestina haikubaliki na kwamba Moscow inataka kuwepo mazingira ya kuanza mazungumzo yanayoweza kutatua mgogoro uliopo.
Katika ujumbe huo Rais Vladimir Putin amesisitiza kuwa, tangu miaka kadhaa iliyopita ulimwengu umeshuhudia njama za kutaka kudhoofisha serikali katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati, kuzidisha matatizo ya kiuchumi na kijamii sambamba na kupanua zaidi makundi yenye mitazamo mikali.
Vilevile amesisitiza kuwa Russia iko tayari kuimarisha uhusiano wake na nchi za Kiarabu kwa ajili ya kupambana na ugaidi.
Mkutano wa kila mwaka wa viongozi wa nchi za Kiarabu umeanza kazi zake leo mjini Nouakchott nchini Mauritania na utaendeleqa hadi kesho.