Israel yafanya mashambulizi mengine makubwa ya anga dhidi ya Syria, yatumia kombora jipya
Utawala wa Kizayuni wa Israel unaendeleza mashambulizi yake makali dhidi ya maeneo mbalimbali ya Syria huku wanamgambo wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi wakiwa wameipindua serikali ya nchi hiyo.
Leo Jumatatu, ndege za kivita za utawala huo zimeshambulia vituo muhimu na miundombinu ya kijeshi katika ukanda wa pwani ya magharibi mwa Syria, ikiwa ni pamoja na miji ya Tartus na Latakia.
Ndege za kivita za Israel zimepiga kwa makombora maghala ya silaha ya maeneo hayo. Miripuko mikubwa imesikika katika miji yote, wakati wa mashambulizi hayo.
Televisheni wa al-Mayadeen ya Lebanon imesema kuwa, vikosi vya Israel vimeingia na kuteka ardhi ya Syria yenye ukubwa wa kilomita 15 katika mkoa wa Quneitra wa magharibi mwa Syria.
Shirika la habari la Sputnik la Russia limeripoti kuwa, mashambulizi ya Israel dhidi ya vituo vya kijeshi huko Hama na Homs, majimbo mengine mawili ya magharibi mwa Syria na kuongeza kuwa, mashambulizi dhidi ya mikoa ya Hama na Halab (Aleppo) ambayo pia iko magharibi mwa Syria yamesababisha maafa makubwa.
Duru mbalimbali za habari zimetangaza kuwa, meli za kivita za Israel zimerusha makombora kadhaa na kupiga maeneo ya pwani ya Syria, hasa mkoa wa Tartus.
Jana Jumapili pia, jeshi la Israel liliteka vijiji vitatu vipya vya Syria, katika mkoa wa Dara'a wa magharibi mwa Syria na vile vile vijiji vya Mazraat Beit Jan na Mughr al-Mir vya Mkoa wa Rif Dimashq.