Marufuku ya Israel dhidi ya shughuli za UNRWA kuanza kutekelezwa leo
Licha ya malalamiko ya walimwengu na asasi muhimu kama Umoja wa Mataifa, lakini utawala wa Israel umekataa kubadilisha uamuzi wake wa kulipiga marufuku Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA)
Utawala wa Kizayuni wa Israel umetangaza kuwa, marufuku ya shughuli za shirika hilo inaanza kutekelezwa leo kama ilivyokuwa imetangaza hapo awali.
Utawala wa Kizayuni wa Israel Ulitangaza tarehe 25 Januari kwamba, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) lina hadi mwisho wa mwezi huu wa Januari kuondoka katika mji mtukufu wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu.
Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon alisema katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kwamba, "UNRWA lazima isitishe shughuli zake huko Jerusalem (Quds), na kuhama majengo yote ambayo inafanyia kazi katika jiji hilo, kabla ya Januari 30, 2025."
Utawala haramu wa Israel umehalalisha hatua yake hiyo kwa kuibua madai yasiyo na msingi kwamba, UNRWA, ambayo imekuwa ikiwasaidia Wapalestina tangu 1949, eti inaajiri wafanyakazi wanaoshiriki katika shughuli za kigaidi.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina limekuwa likisisitiza kuwa, hakuna taasisi yoyote inayoweza kujaza nafasi ya shirika hilo katika kuwahudumia na kuwafikishia misaada wakimbizi wa Kipalestina.
Asasi mbalimbali za kieneo na kimataifa zimesisitiza mara kadhaa kwamba, hakuna shirika linaloweza kuchukua nafasi ya shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, katika Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na vita.