Muqawama mpya wa Syria waanza rasmi, washambulia jeshi la Israel
Kundi moja la Muqawama la Syria limetoa taarifa muhimu ya kijeshi kuhusiana na shambulio la asubuhi ya jana Jumamosi dhidi ya wanajeshi wa Israel katika mashamba ya Quneitra kusini mwa Syria na kutangaza kuanza rasmi Muqawama wa kukomboa ardhi za nchi hiyo zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Sehemu moja ya taarifa ya kijeshi ya Syrian Popular Resistance imesema:
"Katika hatua ya kijasiri inayoonyesha kuwa roho ya Muqawama imekita mizizi katika nyoyo za watu wa Syria, moja ya makundi ya Muqawama ya Syria limefanya operesheni maalumu dhidi ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika mji wa Taranja nje kidogo ya mji wa Quneitra wa kusini mwa Syria."
Hayo yameripotiwa na televisheni ya al Alam ambayo imeendelea kunukuu taarifa ya kijeshi ya Muqawama wa Wananchi wa Syria ikisema: "Baada ya kufanyika mawasiliano na kikundi kilichoendesha operesheni, imethibitishwa kuwa operesheni hiyo ilikuwa ni jibu la haraka na uamuzi uliochukuliwa kwa uhuru kwenye medani ya mapambano, kwani wanamuqawama hao walikuwa wakifuatilia harakati za adui katika eneo hilo na walipopata fursa tu wamewashambulia bila ya kusubiri idhini kutoka juu."
Taarifa hiyo imeendelea kusema: "Adui Mzayuni alijaribu kujibu, lakini wapiganaji wetu walifanya operesheni hiyo kwa kasi na kwa usahihi wa hali ya juu, kisha wakaondoka salama kutoka eneo hilo bila ya kujeruhiwa yeyote kati yao na kuwaacha maadui katika hali ya kuchanganyikiwa. Baada ya hapo jeshi la Israel lilijaribu kulisafisha eneo hilo kwa ajili ya kuwatafuta wahusika wa operesheni hiyo lakini juhudi zao hazikuzaa matunda."
Taarifa hiyo imeendelea kusema: "Muqawama haungojei amri za mtu yeyote katika kila kona ya Syria, bali wanafuatilia kila sekunde nyendo za adui na kuchukua hatua dhidi yake kila wanapopata fursa na mazingira kuruhusu."
Taarifa ya The Syrian Popular Resistance imesisitiza kwamba: "Kila mpiganaji mmoja katika kambi ya Muqawama ni jeshi zima, na kila silaha yake ni risasi katika moyo wa adui na kwamba Wazayuni wavamizi hawatowahi kupata utulivu wowote katika ardhi ya Syria."