Hamas ina uwezo gani wa kujijenga upya?
Ikiwa ni katika kuendelea mwenendo wa kukiri uwezo wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) wa kujikarabati na kujijenga upya, duru za Kizayuni kwa mara nyingine tena zimetangaza kushangazwa na uwezo mkubwa wa kundi hilo la muqawama katika uwanja huo.
Utawala wa Kizayuni uliutwisha Ukanda wa Gaza vita vya zaidi ya miezi 15 ambapo katika kipindi hicho, utawala huo katili ulifanya mauaji ya kimbari ambayo hayajawahi kutokea katika historia dhidi ya watu wa Gaza na vile vile kuharibu kabisa miundombinu yake. Moja ya malengo muhimu ya utawala wa Kizayuni katika vita hivyo vya mauaji ya halaiki lilikuwa ni kuiangamiza kabisa Hamas.
Hivi sasa ikiwa imepita takriban wiki tatu tangu kusitishwa mapigano kati ya utawala wa Kizayuni na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas, dalili za harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Palestina ya kurejesha udhibiti na nafasi yake katika Ukanda wa Gaza zinazidi kudhihiri wazi, kiasi kwamba vyombo vya habari na shakhsia mbalimbali wa Kizayuni wamelazimika kukiri uwezo huo mkubwa.
Elmog Booker, mwandishi wa habari wa Kizayuni amesema katika taarifa yake kwamba: "Inashangaza kuona jinsi Hamas ilivyoweza kujijenga upya katika muda wa saa 72 na kuchukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza." Inaonekana wakati umefika wa kuacha kujisimulia zimulizi zetu wenyewe, Hamas ina udhibiti kamili juu ya Ukanda wa Gaza." Pia, Moshe Bozielov kutoka jopo la kifikra la "Misgav" ambaye pia ni afisa mkuu wa zamani wa shirika la ujajusi la Shabak amesema kuhusiana na suala hili: "Yeyote anayedai kuwa ameishinda Hamas ni muongo." Amir Oyowi, jenerali mstaafu wa jeshi la Kizayuni, pia amekiri kwamba, "tuko katika hali ambayo mchakato wa kuhuisha nguvu ya Hamas unakwenda kwa kasi kubwa kuliko mchakato wa kuangamizwa kwake na jeshi la Kizayuni."
Awali gazeti la Kizayuni la Yediot Aharonot lilisisitiza katika ripoti yake kwamba, matukio ya magwaride ya kijeshi ya Hamas wakati wa kubadilishana mateka hayaachi shaka yoyote kwamba baada ya miezi 15 ya vita, harakati ya Hamas bado inahesabiwa kuwa ni yenye ushawishi mkubwa katika Ukanda wa Gaza. Gazeti hilo pia limekiri likiwanukuu maafisa wa nchi za Magharibi kwamba: "Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Hamas) imeweza kurejesha sehemu kubwa ya uwezo wake wa kusimamia hali ya mambo katika baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Gaza."

Swali muhimu hapa ni kwamba je, Hamas ina uwezo gani wa kujijenga upya? Katika kujibu swali hili, inatosha kutazama uungaji mkono wa Hamas miongoni mwa watu wa Palestina uungaji mkono ambao ulidhihiri wazi baada ya kusimamishwa vita na makaribisho makubwa iliyopewa na wananchi. Uuungaji mkono huo umepelekea Hamas kuweza kusajili wanachama wapya na hivyo kutatua haraka changamoto yake ya upungufu wa nguvukazi. Uwezo mwingine muhimu ni uwepo wa viongozi wanaofaa katika muundo wa nguvu wa Hamas, ambayo licha ya kuwapoteza makamanda wake katika medani ya vita lakini iliweza kuziba pengo hilo haraka na makamanda wengine shupavu. Mohammad Sinwar ni mmoja wa viongozi hao ambao baada ya kuuawa shahidi ndugu yake Yahya Sinwar, alichukua nafasi muhimu katika muundo wa kijeshi wa Hamas, ikiwa ni pamoja na kuajiri wanachama wapya.
Gazeti la Wall Street Journal limetangaza katika ripoti yake kuwa harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Hamas inajenga upya nguvu zake na licha ya mashambulizi makubwa ya utawala wa Kizayuni, imeweza kuvutia wapiganaji wapya. Ripoti hii imetaja jukumu la Mohammad Sinwar, mdogo wake Yahya Sanwar (aliyeuawa shahidi mnamo Oktoba mwaka jana), kuwa lilikuwa la kuongoza mchakato huo. Uwezo mwingine muhimu wa Hamas ni kusimamia masuala ya Ukanda wa Gaza kwa njia ambayo hakuna kundi lolote lingine kati ya makundi ya Palestina lililo na uwezo kama huo.
Kuhusiana na hilo, vyanzo vya habari vimeripoti kuwa Hamas imeweza kuangamiza makundi ya kihalifu yaliyokuwa yakishambulia misafara ya misaada ya kibinadamu na kuipora huku wanajeshi wa Israel wakiwa wanatazama tu bila kuchukua hatua yoyote. Uwezo huo pamoja na uwezo mwingine wa Hamas bila shaka utaushangaza utawala haramu wa Kizayuni utakaposhuhudia kwa karibu maajabu mengine yatakayoibuliwa na Hamas katika siku na miezi ijayo.