Israel kuunda 'wakala wa kuwafukuza' Wapalestina Gaza
Wizara ya Vita ya Israel imesema ipo mbioni kuunda chombo mahsusi cha utawala huo wa Kizayuni cha kushughulikia eti "kuondoka kwa khiari" raia wa Palestina kutoka Gaza.
Televisheni ya al-Jazeera imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, kuundwa kwa wakala huo kunaenda sambamba na mpango uliopendekezwa na Rais wa Marekani, Donald Trump wa kuwahamisha kwa nguvu wakazi wa eneo hilo lililo chini ya mzingiro.
Kadhalika ripoti za vyombo vya habari vya Kizayuni zinasema kuwa, jeshi la utawala huo katili linajiandaa kupokea miili ya mateka wanne waliopelekwa Gaza siku ya Alkhamisi, ikiwa ni sehemu ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Harakati ya Muqawama wa Hamas.
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ameliita pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la "kuitwaa" Gaza "fursa ya kihistoria" ya kudhamini mustakabali wa utawala huo bandia na kudai kwamba kuwaondoa Wapalestina wa Ghaza ndilo "suluhisho pekee linalowezekana."
Netanyahu amedai pia kuwa Israel imo mbioni kuwaondoa Wapalestina katika "eneo la mizozo" la Ghaza, akisisitiza kwamba mpango wa Trump, unaolenga kulinyakua eneo hilo na kuwafukuza wakazi wake, ni mpango pekee ambao yeye Netanyahu anadhani unaweza kuwa na tija.
Jamii ya kimataifa imeendelea kupinga vikali mipango yoyote ya "kuwaondoa kwa nguvu" Wapalestina huko Gaza, na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.