Mamlaka ya Ndani ya Palestina yataka walimwengu waishinikize Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i123418-mamlaka_ya_ndani_ya_palestina_yataka_walimwengu_waishinikize_israel
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeonya juu ya matokeo mabaya ya kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza na kuitaka jamii ya kimataifa kuulazimisha utawala wa Kizayuni utekeleze majukumu yake ya kibinadamu.
(last modified 2025-03-02T22:53:12+00:00 )
Mar 02, 2025 22:53 UTC
  • Mamlaka ya Ndani ya Palestina yataka walimwengu waishinikize Israel

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeonya juu ya matokeo mabaya ya kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza na kuitaka jamii ya kimataifa kuulazimisha utawala wa Kizayuni utekeleze majukumu yake ya kibinadamu.

Katika taarifa yake, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imelaani uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Ukanda wa Gaza na kuonya juu ya madhara ya hatari ya hatua hiyo katika mgogoro wa sasa hususan katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Wizara hiyo imesisitiza kuwa, misaada ya kibinadamu haipaswi kuwa wenzo wa kisiasa; kwa sababu mtazamo huo unazidisha mateso ya Wapalestina zaidi ya milioni 2 ambao tayari walikuwa katika hali mbaya kutokana na vita na mzingiro.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Palestina imeitaka jamii ya kimataifa na pande zote husika kukubali majukumu yao na kuulazimisha utawala wa Kizayuni kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza kwa utulivu na bila vikwazo.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa zaidi ya wanafunzi 100,000 wamejiandikisha mashuleni katika Ukanda wa Gaza baada ya mwaka mpya wa masomo kuanza Februari 23, na kuashiria kurudi mashuleni wanafunzi baada ya muda mrefu wa kusimamishwa masomo kutokana na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kiziayuni wa Israel dhidi ya watu wa eneo hilo la Palestina.