Taarifa ya UN: Israel imetenda Mauaji ya Kimbari Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i123892-taarifa_ya_un_israel_imetenda_mauaji_ya_kimbari_gaza
Ripoti maalum ya Tume Huru ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imebaini kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umetekeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza kwa kuharibu kwa makusudi vituo vya huduma za afya ya uzazi wakati wa mashambulizi yake makali katika eneo hilo.
(last modified 2025-03-14T03:22:02+00:00 )
Mar 14, 2025 03:22 UTC
  • Taarifa ya UN: Israel imetenda Mauaji ya Kimbari Gaza

Ripoti maalum ya Tume Huru ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imebaini kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umetekeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza kwa kuharibu kwa makusudi vituo vya huduma za afya ya uzazi wakati wa mashambulizi yake makali katika eneo hilo.

Ripoti hiyo, iliyotolewa Alhamisi, na Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi kuhusu Maeneo ya Palestina Yaliyokaliwa Kwa Mabavu na Israel, ikiwemo Mashariki mwa Al Quds (Jerusalem), inaeleza aina mbalimbali za ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa dhidi ya wanawake, wanaume, wasichana na wavulana wa Kipalestina tangu Oktoba 7, 2023.

"Utawala wa Israel umeharibu kwa makusudi uwezo wa uzazi wa Wapalestina wa Gaza kama kundi, ikiwa ni pamoja na kuweka vikwazo vinavyolenga kuzuia kuzaliwa kwa watoto, jambo ambalo ni mojawapo ya vitendo vya mauaji ya kimbari kulingana na Mkataba wa Roma na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mauaji ya Kimbari," ilisema ripoti hiyo.

Uchunguzi huo umebaini kuwa Israel imetekeleza angalau vitendo viwili kati ya vitano vinavyotajwa kama mauaji ya kimbari na Umoja wa Mataifa. Mbali na ongezeko la vifo vya wajawazito kutokana na ukosefu wa dawa na vifaa tiba, ripoti hiyo imeeleza kuwa vitendo hivyo ni sawa na uhalifu wa kibinadamu wa maangamizi ya watu.

Ripoti hiyo imesema kuwa Israel inatekeleza sera inayolenga kuathiri maisha ya Wapalestina kwa makusudi kwa njia zinazopelekea kuangamia kwao na kuchukua hatua za kudhibiti uzazi ndani ya jamii hiyo.

"Ukiukwaji huu haujasababisha tu madhara makubwa ya kimwili na kisaikolojia kwa wanawake na wasichana, bali pia umeathiri afya yao ya uzazi kwa muda mrefu, na kupunguza uwezo wa Wapalestina wa kupata watoto kwa siku zijazo," alisema Navi Pillay, Mwenyekiti wa Tume hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Baadhi ya watoto waliouawa katika mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Gaza

Ripoti hiyo ilibaini kuwa Israel ilifanya mashambulizi ya kimfumo dhidi ya hospitali na vituo vya afya vinavyotoa huduma za afya ya uzazi, hali iliyosababisha karibu kusambaratika kabisa kwa sekta ya afya katika Gaza.

Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa vizuizi vikali dhidi ya upatikanaji wa dawa muhimu vimeathiri vibaya afya ya uzazi ya wanawake na wasichana wa Gaza, na kuchangia moja kwa moja ongezeko kubwa la vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

Aidha, ripoti hiyo imelaani vikosi vya Israel kwa kutumia unyanyasaji wa kingono na kuwavua nguo kwa nguvu kama sehemu ya mbinu zao za kuwaadhibu Wapalestina kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa ya Harakati ay Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 2023.

Harakati ya Hamas imetoa taarifa na kusema kuwa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuthibitisha kuwa Israel imetekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina ni uthibitisho wa uhalifu mkubwa wa kibinadamu uliotendeka Gaza wakati wa vita.

“Taarifa ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya watu wa Palestina inathibitisha kile kilichotokea: mauaji ya kimbari na uvunjaji wa haki zote za kibinadamu na sheria za kimataifa,” alisema msemaji wa Hamas, Hazem Qassem.

Kwa msaada wa Marekani na washirika wake wa Magharibi, Israel ilianzisha vita dhidi ya Gaza baada ya Hamas na makundi mengine ya muqawama kushambulia Israel mnamo Oktoba 2023 katika Operesheni Kimbunga cha Al Aqsa, kujibu ukandamizaji wa muda mrefu wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Tangu Oktoba 2023, vita hivyo vimesababisha vifo vya angalau Wapalestina 48,524, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, huku wengine 111,955 wakijeruhiwa.

Makubaliano ya kusitisha mapigano na kubadilishana wafungwa yalitiwa saini tarehe 19 Januari 2024, na kusimamisha mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.