Mwakilishi wa Palestina UN: Israel inaendeleza sera za mauaji ya kimbari
Mwakilishi wa Kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ametuma barua kwa maafisa wa kimataifa akikemea jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Paletina.
Riyad Mansour ametoa barua tatu kwa Rais wa Baraza la Usalama, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na kuendelea sera za mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya watu wa Palestina, ambazo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Mansour ameashiria sera ya Israel ya kutumia njaa kama silaha dhidi ya Wapalestina milioni 2 wa Ukanda wa Gaza kwa kuzuia kuingizwa misaada ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na chakula, maji na huduma za matibabu katika eneo hilo.
Mwakilishi wa Kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa: "Hatua za utawala wa Kizayuni ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya usitishaji vita, azimio la Baraza la Usalama na hatua za muda za Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu. Kulinyima taifa letu mahitaji muhimu ni sehemu ya mauaji ya kimbari."
Riyad Mansour ameashiria hujuma zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa maeneo mengine ya ardhi ya Palestina kama Quds Mashariki na mashambulizi ya utawala huo katika eneo lote la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kusema: "Vitendo hivyo vinadhihirisha sera na mbinu ya wazi inayolenga kufuta kabisa kambi za wakimbizi wa Kipalestina na kuwafukuza kwa nguvu mamilioni ya Wapalestina."
Amesisitiza ulazima wa kusitishwa mauaji ya kimbari ya watu wa Palestina na kuitaka jamii ya kimataifa itekeleze wajibu wake wa kutekeleza utawala wa sheria, kuuadhibu utawala ghasibu wa Israel na kuandaa njia ya ya kisiasa ya kukomesha uvamizi na kufikiwa suluhisho la kuduumu.