Jeshi katili la Israel laendelea kumwaga damu za Wapalestina Gaza
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewaua shahidi Wapalestina wengine 17 katika mashambulizi ya alfajiri ya leo katika Ukanda wa Gaza, siku moja baada ya kuua shahidi Wapalestina zaidi ya 60 akiwemo ripota wa Al Jazeera, Hossam Shabat katika ukanda huo.
Mashambulizi hayo mapya ya wanajeshi wa utawala haramu wa Israel yanajiri siku moja baada ya Wizara ya Afya huko Gaza kusema kwamba, mashambulizi ya Israel kwenye ukanda huo yamesababisha vifo vya Wapalestina 61 katika muda wa saa 24 zilizopita.
Press TV imeripoti kuwa, Ismail Barhoum, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas ameuawa katika moja ya mashambulio hayo alipokuwa akipokea matibabu hospitalini, pamoja na mvulana wa miaka 16.
Katika taarifa yake jana Jumatatu, Wizara ya Afya huko Gaza ilisema miili minne iliopolewa kutoka chini ya vifusi, na kwamba watu 134 waliojeruhiwa kwenye hujuma hizo wamelazwa hospitalini. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vifo vya hivi karibuni vimefikisha idadi ya Wapalestina waliopoteza maisha tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya halaiki ya Israel dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 2023 kupindukia 50,100.

Kadhalika hujuma za Wazayuni zimepelekea kujeruhi Wapalestina wengine 113,408. "Idadi kubwa ya waathiriwa wamesalia chini ya vifusi na mitaani, hawawezi kufikiwa na ambulensi na wafanyakazi wa ulinzi wa raia," wizara imeongeza.
Habari zaidi zinasema kuwa, mbali na mauaji, lakini pia vikosi vya Israel vimewakamata Wapalestina kadhaa, akiwemo mtayarishaji filamu mashuhuri aliyeshinda Tuzo ya Oscar, Hamdan Ballal, baada ya walowezi kuwashambulia na kuwajeruhi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Tangu Machi 18, utawala huo unaendeleza hujuma mpya za kinyama huko Gaza, na kuvunja makubaliano ya usitishaji vita na kubadilishana wafungwa na mateka yaliyodumu kwa karibu miezi miwili.