AP: Yemen imetungua droni 7 za US zenye thamani ya dola milioni 200
Vikosi vya Yemen vimetungua ndege saba zisizo na rubani za Marekani aina ya Reaper katika kipindi cha chini ya wiki sita, na kuisababishia Washington hasara ya zaidi ya dola milioni 200.
Shirika la habari la The Associated Press la Marekani liliripoti habari hiyo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, droni 3 kati ya 7 zilitunguliwa ndani ya wiki iliyopita, hatua inayoonyesha kuboreka kwa uwezo wa vikosi vya Yemen kulenga ndege zisizo na rubani zinazoruka juu ya nchi hiyo kinyume cha sheria.
"Ndege hizo zisizo na rubani zilikuwa zikifanya mashambulizi au kufanya operesheni za kijasusi," wamesema maafisa wa US ambao hawakutaka kutajwa majina.
Ndege hizo za kisasa zisizo na rubani, zilizotengenezwa na kampuni ya General Atomics, zinagharimu takriban dola milioni 30 kila moja, na zina uwezo wa kuruka kwenye mwinuko wa zaidi ya futi 40,000 (mita 12,100) juu ya usawa wa bahari.
Afisa moja wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani ameonya kwamba, kuongezeka kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Yemen kunaweza kuongeza hatari ya kutunguliwa ndege zaidi za US zisizo na rubani.
Haya yanajiri huku Marekani ikishadidisha mashambulizi yake dhidi ya Yemen tangu Rais Donald Trump kuamuru kuchukuliwa "hatua madhubuti ya kijeshi" dhidi ya Yemen. Yemen ilianza tena operesheni za kuiunga mkono Gaza, mwezi uliopita.
Hii ni katika hali ambayo, viwanda vya kutengeza silaha vya Marekani vimezidi kupata hasara kutokana na Yemen kufunga Bahari Nyekundu isitumiwe na meli za Marekani, Israel na chombo chochote cha baharini kinachoupelekea vitu au silaha utawala wa Kizayuni.