Yemen yatwanga tena kambi ya anga ya Israel kwa kombora baada ya shambulio la anga la Marekani
Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree ametangaza kuwa nchi yake imefanya shambulio la kombora dhidi ya kambi ya anga ya jeshi la Israel ili kulipiza kisasi vita vya mauaji ya kimbari vya utawala huo kwenye eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Katika taarifa iliyotolewa mapema leo Ijumaa, Yahya Saree amesema vikosi vya jeshi la Yemen "vimefanya operesheni ya kijeshi na kushambulia kambi ya ndege za kivita ya adui Israel, Ramat David Airbase, mashariki mwa eneo la Haifa linalokaliwa kwa mabavu, kwa kutumia kombora la hypersonic 'Palestine-2' la masafa marefu."
"Kombora hilo limefanikiwa kupiga shabaha yake, shukrani kwa Mungu, na mifumo ya kuzuia makombora imeshindwa kufanya kazi," taarifa hiyo imeongeza.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shambulio hilo limefanyika kwa ajili ya kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa wa Palestina katika vita vya Israel vinavyoungwa mkono na kufadhiliwa na Marekani dhidi ya Gaza.
Saree ameapa kwamba operesheni za kulipiza kisasi zitaendelea hadi vita vya Israel vitakapomalizika na mzingiro uliowekewa kwa watu wa Gaza utakapoondolewa.
Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Yemen imetolewa saa chache baada ya Marekani kushambulia Yemen katika jaribio la kusimamisha operesheni za nchi hiyo zinazoiunga mkono Gaza na kujeruhi watu watatu.