Wanaharakati Bahrain: Hatua yoyote dhidi ya Sh. Qassim italeta maafa
Mwanaharakati mashuhuri wa upinzani na kidini nchini Bahrain ameuonya utawala wa Aal-Khalifa kuwa, hatua yoyote ya kumhujumu Ayatullah Sheikh Isa Qassim, mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu wa nchi hiyo itakuwa na taathira hasi.
Sheikh Abdullah Saleh, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Islamic Action ya Bahrain amesema iwapo utawala wa Manama utaamua kuchukua hatua yoyote ya kumdhuru Sheikh Qassim, kitendo hicho kitasababisha umwagikaji wa damu za raia, ambao wako tayari kujitolea kwa hali na mali kumnusuru kiongozi wao huyo.
Kadhalika ameukosoa utawala wa Aal-Khalifa kwa kutomtambua na kumheshimu Ayatullah Sheikh Isa Qassim, licha ya juhudi zake za kuitisha maandamano ya amani yasiyokuwa ya vurugu. Ofisa huyo wa Islamic Action Society ameifananisha Bahrain na gereza kubwa, kwa namna wananchi hawaruhusiwi kutembea kutoka sehemu moja hadi nyingine wala kutekeleza ibada kwa mujibu wa itikadi zao bila ya idhini kutoka utawala huo wa kifalme.
Haya yanajiri siku chache baada ya utawala wa Manama kuakhirisha kesi dhidi ya Sheikh Isa Qassim, msomi mtajika wa Kiislamu nchini humo iliyotazamiwa kuanza kusikilizwa Jula 27.
Siku moja kabla ya hapo, taarifa ya wanazuoni wa Kiislamu nchini Bahrain ilisema kuwa, mashitaka anayolimbikiziwa Ayatullah Qassim ambaye utawala wa Manama umemvua uraia, ni ya kubuni na wala hayana mashiko na kwamba kesi dhidi yake inakiuka katiba, haki za binadamu zilizoanishwa katika sheria za nchi hiyo na hata za kimataifa.