Kufurushwa au Kufa: UNICEF yakosoa mpango wa Israel wa misaada Gaza
(last modified Sun, 11 May 2025 09:12:09 GMT )
May 11, 2025 09:12 UTC
  • Kufurushwa au Kufa: UNICEF yakosoa mpango wa Israel wa misaada Gaza

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limekosoa vikali mpango tata wa misaada kwa Ukanda wa Gaza unaoungwa mkono na Marekani na Israel, likionya kuwa unaweza kulazimisha familia kuchagua kati ya "kuondoshwa makwao au kufa."

Chini ya mpango huo, uliotangazwa na Balozi wa Marekani katika utawala wa Israel, Mike Huckabee, mfumo wa utoaji misaada utasimamiwa na taasisi binafsi mpya iliyoundwa na Marekani.

Taasisi hiyo inayoitwa Gaza Humanitarian Foundation imepangwa kufungua vituo vya usambazaji misaada ambavyo vitalindwa na wakandarasi binafsi wa kijeshi wa Marekani huku wafanyakazi wa misaada wakihudumu ndani yake.

Umoja wa Mataifa na mashirika mengine makuu ya misaada yanayofanya kazi Gaza yameukataa mpango huo, yakisema hayatashirikiana nao kwani unaonekana “kubadilisha misaada kuwa silaha ya kivita.”

Msemaji wa UNICEF, James Elder, akiwa Geneva, amesema ni “hatari kuwalazimisha raia kuingia katika maeneo yenye ulinzi wa kijeshi ili kuchukua misaada… misaada ya kibinadamu haipaswi kamwe kutumiwa kama njia ya mashinikizo.”

Elder ameonya kuwa kutumia misaada kama “mtego wa kulazimisha watu kuhama, hasa kutoka kaskazini kwenda kusini, kutaleta uamuzi huu mgumu kati ya kulazimishwa kuondoka au kifo.”

Kwa mujibu wa Elder, iwapo mpango huo unaoungwa mkono na Marekani utatekelezwa, watu walio hatarini zaidi Gaza — wazee, watoto wenye ulemavu, wagonjwa na majeruhi wasioweza kusafiri kwenda kwenye vituo vya usambazaji — watakumbana na “changamoto kubwa sana” kupata misaada.

Ameongeza kuwa muundo wa mpango huo “utaongeza mateso yanayoendelea kwa watoto na familia huko Gaza.”

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) iliuelezea mpango huo kama “hautekelezeki kivitendo na hauendani na misingi ya kibinadamu.”

Umoja wa Mataifa pia ulikosoa mpango huo kwa kuwa na idadi ndogo sana ya vituo vya usambazaji, hali ambayo inaweza kulazimisha Wapalestina waliokoseshwa makazi kutembea umbali mrefu wakibeba mizigo mizito ya misaada kwa familia kubwa.

Wapalestina waliouawa katika mauaji ya kimbari yanayoendelezwa na Israel huko Gaza

Shirika Kuu la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetoa wito kwa utawala haramu wa Israel kuondoa mzingiro kamili wa Gaza ambao umedumu kwa karibu wiki 10 badala ya kuanzisha mfumo huo wa misaada, na kuruhusu misaada kuingia bila vizuizi.

UNRWA, ambalo ndilo mtoaji mkubwa wa misaada Gaza, imesema ina zaidi ya malori 3,000 ya misaada ambayo yamekwama nje ya Gaza.

Ukanda wa Gaza umekuwa chini ya kizuizi kamili cha misaada tangu Israel ivunje makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas katikati ya Machi.

Mashirika ya misaada yameonya mara kwa mara kwamba chakula, maji, dawa na mafuta vinakaribia kuisha katika eneo lote lililo na wakazi wengi.

Vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na Israel dhidi ya Gaza vilivyoanza Oktoba 2023 vimesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 52,787  na kujeruhi wengine 119,349. Waathiriwa wengi ni wanawake na watoto.

Mnamo Novemba 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati za kukamatwa kwa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na waziri wa zamani wa vita, Yoav Gallant, kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu huko Gaza.

Tel Aviv pia inakabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutokana na vita vyake dhidi ya Gaza.