Kwa mara nyingine Hamas yashukuru uungaji mkono wa Yemen kwa Ghaza
(last modified Mon, 26 May 2025 10:22:59 GMT )
May 26, 2025 10:22 UTC
  • Kwa mara nyingine Hamas yashukuru uungaji mkono wa Yemen kwa Ghaza

Baada ya vikosi vya Muqawama vya Yemen kufanya shambulio jingine la kombora na kupiga maeneo nyeti na muhhimu ya utawala wa Kizayuni mapema leo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imewashukuru wananchi wa Yemen kwa kuendelea kuwa pamoja na Ghaza na kutoiacha mkono kwa hali yoyote ile.

Harakati ya Hamas imesema: "Tunawashukuru ndugu zetu wa Yemen kwa kuendelea na operesheni zao za kuiunga mkono Ghaza. Shambulio la hivi karibuni zaidi yaani shambulio la kombora la leo (Jumapili) kwenye Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion wa utawala wa Israel, limetupa faraja kubwa."

Sehemu nyingine ya taarifa ya Hamas imesema: "Operesheni hiyo ya uungaji mkono wa Yemen kwa watu wa Ghaza inaakisi misimamo adhimu na mitukufu ya taifa rafiki na ndugu la Yemen, ambalo umbali wa masafa haujawazuia kuliunga mkono kivitendo taifa la Palestina."

Kabla ya hapo Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa Majeshi ya Yemen, alikuwa ametangaza leo Jumapili kwamba, kikosi cha makombora cha Yemen kimefanya operesheni maalumu ya kijeshi dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Jaffa la Tel Aviv kwa kutumia kombora la kisasa la balestiki.

Ameongeza kuwa: "Operesheni hiyo mefanyika kwa mafanikio na kusababisha mamilioni ya Wazayuni kukimbilia kwenye mashimo ya kujifichia na uwanja wa ndege umefungwa."

Msemaji wa jeshi la Yemen ameeleza kuwa, mauaji ya kila siku huko Ghaza yanaisukuma Yemen kwenye kushadidisha operesheni za kijeshi (dhidi ya utawala wa Kizayuni) na mashambulio hayo ya kulipiza kisasi hayatosimama hadi pale Israel itakapositisha kikamilifu jinai zake huko Ghaza.