Jordan yawashutumu walowezi wa Israel kuingia kwa nguvu Al-Aqsa
Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Wageni ya Jordan imelaani vikali vitendo vya mara kwa mara vya walowezi wa Kizayuni kuvamia Msikiti wa Al-Aqsa.
Katika taarifa yake jana Jumanne, wizara hiyo imesisitiza kuwa Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Jordan ndiyo mamlaka pekee yenye jukumu la kusimamia na kudhibiti masuala ya Masjidul Aqsa.
Siku za Jumatatu na Jumanne, mamia ya walowezi wa Israel waliingia kwa nguvu kwenye Kiwanja cha Msikiti wa Al-Aqsa huko al-Quds inayokaliwa kwa mabavu, kusherehekea sikukuu ya Kiyahudi ya Shavuot, inayojulikana pia kama Sikukuu ya Wiki.
Kwa mujibu wa walioshuhudia, Walowezi hao wa Kizayuni walifanya matambiko ya uchochezi ya Talmudi kwenye lango la Msikiti wa Aqsa, kuadhimisha sikukuu ya Kiyahudi ya Shavuot.
Zaidi ya walowezi 12,000 wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada wamevamia msikiti mtakatifu wa al-Aqswa mwezi Mei pekee uliomalizika na kufanya vitendo vya kichochezi katika eneo hilo takatifu.
Kwa mujibu wa duru za Palestina, mwezi Mei 2025, walowezi 12,378 wa Kizayuni walivamia msikiti wa Al-Aqsa kwa visingizio mbalimbali vikiwemo vya utalii na kuungwa mkono na serikali inayoikalia kwa mabavu na vikosi vyake vya usalama.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua.