Hamas: Veto ya Marekani ni kuipa idhini Israel kufanya uhalifu zaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i127218-hamas_veto_ya_marekani_ni_kuipa_idhini_israel_kufanya_uhalifu_zaidi
Harakati za HAMAS na Jihadul Islami za Palestina zimetoa taarifa za kulaani vikali hatua ya Marekani ya kutumia kura ya turufu katika Baraza la Usalama na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni kuzidi kuipa idhini Israel ifanye jinai kubwa zaidi.
(last modified 2025-06-05T12:41:31+00:00 )
Jun 05, 2025 12:41 UTC
  • Hamas: Veto ya Marekani ni kuipa idhini Israel kufanya uhalifu zaidi

Harakati za HAMAS na Jihadul Islami za Palestina zimetoa taarifa za kulaani vikali hatua ya Marekani ya kutumia kura ya turufu katika Baraza la Usalama na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni kuzidi kuipa idhini Israel ifanye jinai kubwa zaidi.

Katika taarifa yake, HAMAS imesema: "Kura ya turufu ya Marekani ni kielelezo cha uungaji mkono wa kibubusa wa Washington kwa serikali ya kifashisti ya utawala unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na ina maana ya kuunga mkono jinai za utawala huo dhidi ya binadamu."

Ikionesha masikitiko kutokana na kitendo cha serikali ya Marekani cha kutojali sheria za kimataifa, HAMAS imesisitiza kuwa: "Marekani imeonesha kuwa haiheshimu sheria za kimataifa kutokana na kupinga kwake juhudi za kimataifa za kukomesha kabisa umwagaji damu huko Palestina."

Harakati hiyo Mapambano ya Kiislamu ya Palestina aidha imesema: "Wanachama 14 kati ya 15 wa Baraza la Usalama wameunga mkono kusitishwa vita vya mauaji ya umati huko Ghaza, lakini ni Marekani pekee ndiyo iliyopinga azimio hilo kwa kutumia kura ya veto."

HAMAS imeonya kwa kusema: "Msimamo huo wa Marekani ni sawa na kumpa idhini mhalifu wa kivita, Benjamin Netanyahu - ambaye anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu - kuendeleza mauaji ya kikatili dhidi ya watu wetu."

Imegusia pia kushindwa Baraza la Usalama kukomesha mauaji ya kimbari na ya umati na kuvunja mzingiro wa Ghaza tangu mwaka 2000, na kusema: “Kushindwa huko kunazua maswali ya kimsingi kuhusu jukumu la taasisi za kimataifa na ufanisi wa sheria na mikataba ya kimataifa.”

Mwisho HAMAS imeitaka jamii kimataifa kuchukua hatua za haraka za kuzuia kuporomoka vibaya mno maadili ya kibinadamu na kushinikiza kusitishwa mara moja vita vya mauaji ya kimbari na kuburuzwa mahakamani viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa jinai zao dhidi ya wananchi wa Palestina.

Kwa upande wake, harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imetoa taarifa tofauti na kusema: "Kura ya Veto ya Marekani inathibitisha bila shaka yoyote kwamba serikali ya Marekani ni muungaji mkono wa moja kwa moja wa jinai zinazofanywa na serikali ya mhalifu wa kivita, Benjamin Netanyahu."