Afisa wa Syria aonya: Yumkini Israel imetuvamia ili kumpindua al-Sharaa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128502-afisa_wa_syria_aonya_yumkini_israel_imetuvamia_ili_kumpindua_al_sharaa
Afisa mmoja wa Syria amesema Israel imeishambulia Syria kwa kisingizio cha kuwalinda wafuasi wa jamii ya Druze walio wachache huko Suwayda, lakini nia ya hasa ni kupindua serikali ya Syria inayoongozwa na Rais wa mpito, Ahmed al-Sharaa.
(last modified 2025-10-17T05:53:46+00:00 )
Jul 19, 2025 06:18 UTC
  • Afisa wa Syria aonya: Yumkini Israel imetuvamia ili kumpindua al-Sharaa

Afisa mmoja wa Syria amesema Israel imeishambulia Syria kwa kisingizio cha kuwalinda wafuasi wa jamii ya Druze walio wachache huko Suwayda, lakini nia ya hasa ni kupindua serikali ya Syria inayoongozwa na Rais wa mpito, Ahmed al-Sharaa.

Tarek Ahmad, mwanachama wa chama cha Syrian Social Nationalist Party, amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik na kuongeza kuwa, "Pengine Israel ilimuwekea mtego Ahmad Sharaa. Huenda walimhadaa kwa kumuonyesha mustakabali wenye matumaini makubwa, na kuahidi kuwa kila kitu kitakuwa sawa ikiwa atatia saini makubaliano ya amani. Donald Trump alikutana naye na ahadi zingine pia zilitolewa."

Afisa huyo wa Syria ameendelea kubainisha kuwa, baada ya kukutana na Trump, Sharaa alijihisi amepata faraja, akidhani angeweza kuwatuma waasi na askari wake kwenye jimbo la Suwayda, na hivyo ndivyo akawa ameingia mtegoni. Sasa, Israel imepata fursa ya kupiga mabomu sio tu Suwayda lakini pia Damascus na kupigana na askari wake."

Haya yanajiri huku Israel ikishadidisha mashambulizi yake mapya dhidi ya Syria, ambapo mashambulizi ya karibuni yalilenga lango la makao makuu ya jeshi katika mji mkuu, Damascus. Vyombo vya habari vya Israel vimetaja mashambulizi hayo kuwa 'ujumbe' kwa kiongozi wa mpito wa Syria, Ahmed al-Sharaa, maarufu kama Abu Mohammad al-Jolani.

Israel inadai kufanya hujuma hizo eti kuwaunga mkono watu wa jamii ya wachache wa Druze nchini Syria, ambao Tel Aviv inawaona kama waitifaki wake watarajiwa katika nchi hiyo ya Kiarabu iliyokumbwa na mgogoro. 

Bunge la Waarabu limelaani vikali mashambulizi hayo ya Israel dhidi ya Syria, na kutangaza kuwa huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na tishio kubwa kwa utulivu wa kikanda.