Njaa, utapiamlo vyaua Wapalestina 86 katika Ukanda wa Gaza
Wizara ya Afya ya Gaza imesema athari hasi za mzingiro wa kibaguzi wa Israel dhidi ya ukanda huo zimesababisha makumi ya Wapalestina kuaga dunia.
Takriban watu 86 huko Gaza, wakiwemo watoto 76 na watu wazima 10, wamefariki dunia kutokana na njaa na utapiamlo, kufuatia mzingiro na vizuizi vya Israel kwenye eneo hilo, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.
Katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram, Wizara ya Afya ya Gaza imesema, kiwango cha njaa na utapiamlo katika eneo hilo kinasababisha "mauaji ya kimya kimya."
"Wizara ya Afya inabebesha [Israel] na jumuiya ya kimataifa dhima (kwa vifo hivyo). Tunataka kufunguliwa mara moja kwa vivuko ili kuruhusu chakula na dawa kuingia," wizara hiyo imesema.
Wakati huo huo, jeshi katili la Israel limeendelea kuwaua Wapalestina wenye njaa, wakiwa katika safu za kupokea msaada wa chakula.
Watu wasiopungua 84 wakiwemo 73 waliokuwa wakitafuta misaada ya kibinadamu, waliuawa kwenye mashambulizi ya Israel kote Gaza jana Jumapili pekee. Zaidi ya watu 200 walijeruhiwa pia.
Wapalestina wengine wawili, ikiwa ni pamoja na mtoto mchanga wa siku 35, wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na utapiamlo katika Hospitali ya al-Shifa ya jiji la Gaza.