Israel yaendelea kumwaga damu za wanahabari Gaza, yaua wengine 4
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129980-israel_yaendelea_kumwaga_damu_za_wanahabari_gaza_yaua_wengine_4
Kwa akali wanahabari wanne wa Kipalestina, akiwemo mpiga picha wa televisheni ya Al-Jazeera, ni miongoni mwa watu 15 waliouawa shahidi katika shambulio jipya la Israel dhidi ya hospitali moja iliyoko kusini mwa Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-08-25T10:36:07+00:00 )
Aug 25, 2025 10:36 UTC
  • Israel yaendelea kumwaga damu za wanahabari Gaza, yaua wengine 4

Kwa akali wanahabari wanne wa Kipalestina, akiwemo mpiga picha wa televisheni ya Al-Jazeera, ni miongoni mwa watu 15 waliouawa shahidi katika shambulio jipya la Israel dhidi ya hospitali moja iliyoko kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Inaarifiwa kuwa, ndege isiyo na rubani ya Israel ilishambulia dari ya paa la Hospitali ya Nasser na kuua shahidi mwandishi mmoja wa habari; hujuma iliyofuatiwa na shambulio la anga la utawala huo wa Kizayuni lililoa shahidi wanahabari wengine watatu.

Habari zaidi zinasema kuwa, mashambulizi hayo yameua takriban watu 15, wakiwemo waandishi wa habari wanne na mfanyakazi mmoja wa uokoaji, kwa mujibu wa maafisa wa afya wa Palestina.

Waliouawa shahidi ni pamoja na Mohammed Salama wa televisheni ya Al-Jazeera ya Qatar, Hossam al-Masri wa shirika la habari la Reuters, mwandishi wa habari wa mtandao wa NBC, Moaz Abu Taha na mwanahabari wa kujitegemea, Mariam Abu Daqa.

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa maoni na kujieleza, Irene Khan, amesema kuwa jeshi la Israel linataka "kuua ukweli" kwa kunyamazisha kila sauti inayosimulia kile kinachotokea katika Ukanda wa Gaza.

Anasisitiza kuwa, kutokuadhibiwa na kuwawajibisha viongozi wa Israel kwa mauaji ya makumi ya maelfu ya watu wa Gaza, wakiwemo mamia ya waandishi wa habari, kunaihamasisha Israel kuendeleza mauaji, na ametoa wito wa kuongezwa mashinikizo na vikwazo dhidi ya Tel Aviv.

Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Gaza imesema takriban waandishi wa habari 244 na wafanyakazi wa vyombo vya habari sasa wameuawa kwenye mashambulizi ya Israel kote Gaza tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya halaiki mnamo Oktoba, 2023. 

Kwa mujibu wa Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ), kati ya zaidi ya raia 62,000 walioripotiwa kuuawa shahidi na vikosi vya Israel huko Gaza mpaka sasa, zaidi ya 278 walikuwa waandishi wa habari.