Wabahrain waendelea kukusanyika mbele ya nyumba ya Sheikh Issa Qassim
Wananchi wa Bahrain wanaendelea kukusanyika mbele ya nyumba ya kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia wa nchi hiyo Ayatullah Sheikh Issa Qassim licha ya hali ya hewa ya joto kali iliyoko nchini humo hivi sasa.
Siku 50 zimepita tangu wananchi wa Bahrain waanze kukusanyika kandokando ya nyumba ya Sheikh Issa Qassim katika eneo la Al-Daraz, magharibi mwa mji mkuu Manama katika anga ya joto kali; pamoja na hayo jibu la utawala wa Aal Khalifa kwa mkusanyiko huo limekuwa ni kuendeleza mzingiro na kuwatia nguvuni shakhsia na maulamaa wa kidini.
Wananchi wa Bahrain wanataka kusimamishwa vitendo vya hujuma dhidi ya Waislamu wa Kishia na kupewa ulinzi na hifadhi kiongozi wa Waislamu hao Ayatullah Sheikh Issa Qassim.
Wakati huohuo vikosi vya usalama vya utawala huo wa Kifalme, leo asubuhi vimemtia nguvuni Sheikh Aziz Hassan Al-Khadhran.
Hapo jana utawala wa Aal Khalifa ulimtia nguvuni Sheikh Imad Al-Sha'lah, Sayyid Yasin al-Musawi na Sheikh Hussein al- Mahrus.
Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, watu 149 wakiwemo shakhsia na maulamaa wa kidini wameitwa kusailiwa na maafisa usalama wa utawala wa Aal Khalifa huko nchini Bahrain.../