Waziri Mkuu wa Qatar: Benjamin Netanyahu anapasa 'kufikishwa mbele ya sheria'
Waziri Mkuu wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani amelaani mashambulizi ya juzi ya Israel dhidi ya Doha na kuyataja kuwa ni "ugaidi wa kiserikali,". Amesema kuwa Waziri Mkuu wa utawala wa Israel Benjamin Netanyahu anapasa "kufikishwa mbele ya sheria."
Netanyahu jana Jumatano aliituhumu Qatar kuwa inawasaidia na kuwahami magaidi. "Ninaiambia Qatar na mataifa yote yanayowahifadhi magaidi, ima uwafukuze au uwafikishe kwenye vyombo vya sheria kwa sababu usipofanya hivyo, tutafanya hivyo, " amesema Netanyahu.
Akijibu matashi haya ya Waziri Mkuu wa Israel, Waziri Mkuu wa Qatar amesema: " Hatukubali tishio kama hilo kutoka kwa mtu kama Netanyahu… anahitaji kufikishwa mahakamani, yeyendiye anayetafutwa na Mahakama ya ICC.”
Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani amesisitiza kuwa Marekani na Israel walifahamu vyema kuhusu uwepo viongozi wa Palestina huko Doha kwa ajili ya kujadili makubaliano na kwamba viongozi wa Marekani na Israel miaka kadhaa sasa wamekuwa wakiitumia Qatar kama njia ya mawasiliano kwa ajili ya Gaza.
Waziri Mkuu wa Qatar ameongeza kusema: Shambulio dhidi ya mamlaka ya kujitawala Qatar limevuka "kiwango cha chini sana cha adabu na maadili," na kwamba Marekani iliiarifu nchi yake kwa kuchelewa sana.
Mohammed bin Abulrahman bin Jassim Al Thani pia ameeleza kuwa utawala wa Israel umeuwa matumaini kwa mateka waliosalia huko Gaza.
Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imetoa taarifa na kulaani matamshi ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni. Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imeyataja matamshi ya Benjamin Netanyahu kuwa ni hatua ya fedheha kwa ajili ya kujaribu kuhalalisha shambulio la woga ambalo dhidi ya Qatar.
Inafaa kuashiria hapa kuwa Qatar imekuwa mpatanishi katika mazungumzo kati ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na Israel.
Jana pia Netanyahu alitishia tena kuwauwa viongozi wa Hamas huko Qatar iwapo Doha haitawafukuza viongozi wa harakati hiyo.