Jeshi la Israel laua Wapalestina wanne waliokuwa wakitafuta msaada Gaza, njaa yashadidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130766-jeshi_la_israel_laua_wapalestina_wanne_waliokuwa_wakitafuta_msaada_gaza_njaa_yashadidi
Jeshi la Israel limefyatua risasi dhidi ya kundi la Wapalestina waliokuwa wakitafuta msaada wa kibinadamu huko Gaza, na kuwaua angalau watu wanne, huku hospitali katika eneo hilo lilozingirwa zikiripoti vifo zaidi vinavyotokana na njaa na utapiamlo.
(last modified 2025-09-13T23:13:02+00:00 )
Sep 13, 2025 23:13 UTC
  • Jeshi la Israel laua Wapalestina wanne waliokuwa wakitafuta msaada Gaza, njaa yashadidi

Jeshi la Israel limefyatua risasi dhidi ya kundi la Wapalestina waliokuwa wakitafuta msaada wa kibinadamu huko Gaza, na kuwaua angalau watu wanne, huku hospitali katika eneo hilo lilozingirwa zikiripoti vifo zaidi vinavyotokana na njaa na utapiamlo.

Shirika rasmi la habari la Palestina, WAFA, likinukuu vyanzo hivyo, liliripoti kuwa wanajeshi wa Israel waliwalenga moja kwa moja raia waliokuwa katika eneo la Wadi Gaza, katikati mwa Gaza, siku ya Jumamosi. Wengine kadhaa walijeruhiwa katika tukio hilo la ufyatuaji risasi.

Tukio hili linajiri wakati ambapo zaidi ya Wapalestina 1,000 waliokuwa wakitafuta msaada wameuawa na jeshi la Israel karibu na vituo vya usambazaji wa misaada vinavyoendeshwa na shirika linaloitwa Gaza Humanitarian Foundation (GHF), linaloungwa mkono na Marekani na Israel, ambalo lilianza shughuli zake mwishoni mwa Mei.

GHF limekumbwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kibinadamu kwa kushindwa kutoa msaada wa kutosha na kwa hali mbaya ya usalama katika na karibu na vituo vyake vya usambazaji wa misaada.

Mashirika ya misaada na mamlaka za afya zimeonya kuhusu ongezeko kubwa la njaa, hasa miongoni mwa watoto na wazee. Licha ya mahitaji yanayoongezeka, kiwango cha msaada kinachoingia Gaza bado kiko chini sana ya kile kinachohitajika.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Gaza inahitaji angalau malori 500 hadi 600 ya misaada kwa siku ili kukidhi mahitaji ya msingi ya kibinadamu.

Pia siku ya Jumamosi, mashambulizi ya anga ya Israel yalilenga shule ya Umoja wa Mataifa iliyokuwa ikihifadhi Wapalestina waliopoteza makazi yao katika Jiji la Gaza. Jengo la makazi lenye ghorofa nyingi lililipuliwa na kuharibiwa kabisa.

Israel imekuwa ikiharibu majengo marefu katika Jiji la Gaza, ambapo imebomoa kikamilifu mtaa mzima uliokuwa ukiwahifadhi maelfu ya wakazi. Idara ya Ulinzi wa Raia wa Palestina imeripoti kuwa angalau majengo 50 yenye ghorofa yamebomolewa katika wiki za hivi karibuni, sambamba na kuongezeka kwa uhamishaji wa kulazimishwa.

Baadhi ya mitaa imeharibiwa karibu kabisa. Katika eneo la Zeitoun, zaidi ya nyumba na miundo mbinu 1,500 zimeangamizwa tangu mwanzo wa Agosti, na kusababisha sehemu za eneo hilo kubaki bila jengo lolote lilosimama.

Jeshi la Israel limeendeleza mashambulizi makali dhidi ya Gaza tangu Oktoba 7, 2023, likipuuzilia mbali miito ya kimataifa ya kusitisha mapigano, na kusababisha vifo vya angalau Wapalestina 64,756, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Mashambulizi ya anga yasiyokoma yameharibu vibaya eneo hilo na kusababisha uhaba mkubwa wa chakula.