Tangu ulipotangazwa usitishaji vita Ghaza, Israel imewaua shahidi Wapalestina wasiopugua 386
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134172-tangu_ulipotangazwa_usitishaji_vita_ghaza_israel_imewaua_shahidi_wapalestina_wasiopugua_386
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Habari ya Ukanda wa Ghaza ametangaza kuwa jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel halijaheshimu wala kufungamana na makubaliano ya kusitisha mapigano na itifaki ya masuala ya kibinadamu iliyoainishwa kwenye makubaliano hayo.
(last modified 2025-12-11T09:09:33+00:00 )
Dec 11, 2025 07:12 UTC
  • Tangu ulipotangazwa usitishaji vita Ghaza, Israel imewaua shahidi Wapalestina wasiopugua 386

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Habari ya Ukanda wa Ghaza ametangaza kuwa jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel halijaheshimu wala kufungamana na makubaliano ya kusitisha mapigano na itifaki ya masuala ya kibinadamu iliyoainishwa kwenye makubaliano hayo.

Ismail Al-Thawabet, amebainisha kuwa, hali ya kibinadamu katika eneo hilo inazidi kuwa mbaya sambamba na kuwadia msimu wa baridi kali na mvua.

Al-Thawabet ameeleza kwamba uchokozi unaoendelea kufanywa na utawala ghasibu wa Israel wa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano hadi sasa umepelekea kuuawa shahidi Wapalestina wasiopungua 386.

Amesema, kwa mujibu wa makubaliano hayo, mahema na nyumba za dharura 250,000 zilikuwa zipelekwe Ukanda wa Ghaza wakati huu ambapo kuna familia 288,000 ambazo zimebaki bila makazi.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Habari ya Ghaza ameongeza kuwa, malori 6,000 yaliyobeba misaada yamekwama kwenye vivuko vya mpaka; na jeshi vamizi la kizayuni haliyaruhusu kuingia kwenye eneo hilo.

Al-Thawabet amesema: "tunatoa wito kwa ulimwengu, Trump na Baraza la Usalama kuwashinikiza wavamizi".

Kuhusiana na suala hilo, Shirika la Ulinzi wa Raia la Ghaza limetangaza kwamba limepata miili mingine zaidi ya 30 ya Wapalestina waliouawa shahidi kutoka kwenye kaburi la halaiki katika Kituo cha Matibabu cha Shafa.

Shirika hilo limebainisha kuwa, operesheni ya kufukua miili hiyo inaendelea na inakadiriwa kwamba idadi ya waliouawa shahidi waliozikwa katika Kituo cha Matibabu cha Shafa inapindukia 300.

Japokuwa makundi ya Muqawama ya Palestina hadi sasa yameshawakabidhi mateka wote wa Kizayuni walio hai na miili ya waliofariki isipokuwa mwili mmoja tu, huku juhudi za kuutafuta zikiwa zinaendelea, utawala wa Kizayuni haujafungua vivuko vya mpakani wala kuruhusu bila kuweka mpaka uingizaji wa misaada na vifaa vya makazi huko Ghaza.

Utawala wa Kizayuni unakataa pia kuingia kwenye awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha vita kwa kisingizio cha kubaki mwili wa mfungwa mmoja tu wa Kizayuni ambao haujakabidhiwa.../