Israel na walowezi wa Kizayuni wazidisha mashambulizi katika Ukingo wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i138942-israel_na_walowezi_wa_kizayuni_wazidisha_mashambulizi_katika_ukingo_wa_magharibi
Wanajeshi wa Israel na walowezi wa Kizayuni wamezidisha mashambulizi yao dhidi ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2026-06-07T03:20:29+00:00 )
Jun 07, 2026 03:18 UTC
  • Askari wa Israel wakishambulia vijiji vya Wapalestina
    Askari wa Israel wakishambulia vijiji vya Wapalestina

Wanajeshi wa Israel na walowezi wa Kizayuni wamezidisha mashambulizi yao dhidi ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu.

Wizara ya Afya ya Palestina imeripoti kuwa matukio ya ufyatuaji risasi yalijiri siku ya Jumamosi katika mji wa al-Khalil, ambapo mtoto mchanga alipoteza maisha muda mfupi baada ya kupigwa risasi.

Katika hujuma nyingine, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, walowezi wa Kizayuni waliwashambulia na kuwateka nyara wakulima kadhaa wa Kipalestina katika kijiji cha Atuf, kusini mashariki mwa Tubas.

Afisa mmoja katika Ukingo wa Magharibi ameeleza kuwa washambuliaji hao walikuwa wamevalia sare za kijeshi za Israel.

Huko Deir Dibwan, mashariki mwa mji wa Ramallah, wanajeshi wa Israel walivamia nyumba ya familia ya Wapalestina huku wenye nyumba wakipambana kuwazuia walowezi wa Kizayuni kuingia katika nyumba yao.

Watu walioshuhudia wamesema kuwa, wanajeshi wa utawala wa Israel waliwafungia watu wa nyumba hiyo kwenye chumba kimoja na kuwaamuru kuondoa kamera zilizokuwa zikirekodi uvamizi wa Israel.

Ripoti ya Kamisheni ya Palestina dhidi ya Ujenzi wa Vitongoji vya Walowezi wa Kizayuni na Ukuta wa Kibaguzi wa Israel (CWRC) imeeleza kuwa mwaka jana ulikuwa "mwaka wa umwagaji damu" katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu ambapo Israel na walowezi wa Kizayuni walifanya mashambulizi 23,800 dhidi ya Wapalestina.